Khadija Dalasia - Nkasi ,Rukwa
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere, leo Julai 21,2025 ameongoza kikao kazi na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi na kutoa pongezi kwa usimamizi thabiti wa miradi ya maendeleo, hususan kwenye sekta za Afya, Elimu na Maji.
Katika kikao hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri, Mheshimiwa Makongoro aliwapongeza watumishi hao kwa kuonesha mshikamano, uwajibikaji na moyo wa kizalendo katika utekelezaji wa majukumu yao, hali iliyowezesha miradi ya maendeleo kukamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa. “Ninawapongeza sana kwa kazi nzuri mnayoifanya. Miradi yetu ya Afya, Elimu na Maji inatekelezwa vizuri na inakamilika kwa wakati. Huu ni ushahidi tosha wa usimamizi bora na umoja miongoni mwenu,” alisema Mheshimiwa Makongoro.
Aidha, Mkuu wa Mkoa amewataka kuendeleza moyo wa kujituma, kushirikiana kwa karibu na kuhakikisha wananchi wananufaika moja kwa moja na miradi hiyo kwa kupata huduma bora, zenye tija na zinazogusa maisha yao ya kila siku. Kikao hicho ni sehemu ya ziara ya kikazi ya Mkuu wa Mkoa kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuzungumza na watumishi wa umma katika halmashauri zote za mkoa wa Rukwa.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa amekagua miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa shule ya Msingi Chima, ujenzi wa madarasa na mabweni katika shule ya Sekondari Chala, ujenzi wa shule ya amali ya wilaya Londokazi, ujenzi wa shule ya amali ya Mkoa iliyopo kata ya Majengo,ujenzi wa shule mpya ya Sekondari Kata ya Isunta, ukamilishaji wa nyumba za watumishi katika Hospitali ya Wilaya ya Nkasi.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa