Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Charles Makongoro Nyerere ametaka matokeo ya Sensa 2022 yatumike katika kupanga na kutoa huduma kwa wananchi.
Mheshimiwa Makongoro ameyasema hayo leo Agosti 20, 2024 katika ukumbi wa Nazareth mjini Sumbawanga alipokuwa akifungua mafunzo ya usambazaji na uhamasishaji matumizi ya matokeo ya Sensa 2022 kwa Viongozi na Watendaji wa Mkoa wa Rukwa.
Mkuu wa Mkoa amesema lengo la Sensa duniani kote ni kupata takwimu za msingi za watu na hali zao za makazi ili zitumike kufanya maamuzi, kutunga sera, kupanga na kufuatilia mipango ya utekelezaji. Ametaka viongozi na watendaji wa Mkoa wa Rukwa kufanya matumizi sahihi ya takwimu hizo kwa ajili ya maendeleo ya watu.
Akihitimisha hotuba yake ya ufunguzi wa mafunzo hayo Mheshimiwa Makongoro ametoa maelekezo kuwa matokeo ya Sensa 2022 yasambazwe na kubandikwa katika ofisi za Kata, Vijiji, Vitongoji na Mitaa.
Maelekezo mengine yaliyotolewa ni pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri kufanya matokeo ya Sensa na matumizi ya takwimu hizo kuwa agenda ya kudumu katika vikao vya Halmashauri.
Aidha Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa ameeleza kuwa zoezi la anuani za makazi ni endelevu na hivyo kutaka kuwekwa kwa mipango ya uendelezaji wa zoezi hilo.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa amehitimisha hotuba yake kwa kusisitiza umuhimu wa kupokelewa kwa maoni ya wananchi katika kipindi ambacho maandalizi ya Dira ya Maendeleo 2050 yanaendelea.
Semina hiyo imehudhuriwa na timu ya maafisa kutoka Ofisi ya Takwimu ya Taifa ikiongozwa na Bw. Oscar Mangula
Mwakilishi wa Mtakwimu Mkuu wa Serikali ambaye amekabidhi ramani ya Mkoa wa Rukwa na Halmashauri inayoonesha idadi ya watu kulingana na matokeo ya Sensa 2022 itakayotumika kama mwongozo katika upangaji wa maendeleo na kufanya maamuzi katika Mkoa wa Rukwa
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa