Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Charles Makongoro Nyerere amezitaka Taasisi za Umma ambazo zinahudumiwa na TEMESA kufanya malipo kwa wakati ili kuiwezesha taasisi hiyo kutoa huduma endelevu.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa ameeleza hayo leo tarehe 21 Novemba 2023 alipokuwa akifungua kikao kati ya TEMESA na wadau wake Mkoani Rukwa kilichofanyika katika ukumbi wa Nazareth, Sumbawanga.
Mheshimiwa Makongoro amesema pamoja na malalamiko ya ucheleweshwaji wa matengenezo ya mitambo hasa magari, gharama kubwa za matengenezo, matengenezo chini ya kiwango, uchakavu wa karakana na vitendea kazi, mafundi kukosa ujuzi, weledi na uaminifu TEMESA imeendelea kufanyiwa maboresho akieleza kuwa Serikali imetoa fedha kwa TEMESA kwa ajili ya ukarabati wa karakana na ununuzi wa vitendea kazi.
Imeelezwa kuwa tayari maboresho yameanza kwa ukarabati wa karakana, ununuzi wa vifaa vya kisasa na wataalamu kupelekwa masomoni.
Mheshimiwa Makongoro amesema ana imani kuwa maboresho yanayofanywa na Serikali yataleta tija iliyokusudiwa na kupunguza ama kuondoa kabisa malalamiko ya wateja wanaohudumiwa na TEMESA huku akiwataka watendaji wa taasisi hiyo kuendana na maboresho yanayofanywa.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa