Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ameusisitiza umoja wa wazee mkoani Rukwa kuendelea kuhimiza malezi bora katika jamii ili kujiepusha na uvunjifu wa amani unaofanywa na vijana hao pindi wasiposimamiwa vizuri katika makuzi yao.
Amesema kuwa uhalifu mwingi unaoendelea katika maeneo mbalimbali ya nchi hufanywa na kundi la vijana ambao wamekosa usimamizi bora wa malezi ya jamii katika makuzi yao na hatimae hujihusisha na matukio yanayopelekea kuitikisa amani ya mji ama mkoa.
“Uhalifu mwingi nchini hufanywa na kundi la vijana sijawahi kusikia uhalifu umefanywa na kundi la wazee hata siku moja na yote hayo ni kukosa malezi bora kutoka kwenu wazee, kama wazee mlilelewa vizuri kwanini na hawa watoto, au mmewashindwa?” Aliuliza.
RC Wangabo ameyasema hayo alipofanya kikao na umoja wa wazee wa mkoa wa Rukwa pamoja na viongozi wa dini kilichofanyika katika ikulu ndogo Mkoani humo na kuwaeleza mikakati aliyonayo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha amani na utulivu unaendelea kudumishwa katika mkoa.
Aidha, RC Wangabo amesisitiza kuwa vijana wamekuwa wakijifunza mambo mengi machafu kupitia simu za “smartphone” ikiwemo namna ya kufanya uhalifu na mambo yanayokwenda kinyume na maadili ya mtanzania.
Ameonya kuwa baadhi ya wazazi hutetea uovu wa watoto wao jambo linalowakatisha tamaa waalimu katika kujenga maadili ya wananfunzi ili kutengeneza viongozi bora katika jamii na kuongeza kuwa watoto wasio na maadili hushusha kasi ya ufaulu mashuleni.
RC Wangabo hakuacha kuwashauri wazee hao kuacha kujishughulisha na siasa za maandamano na badala yake wawe washauri wa vijana wanaotaka kuharibu amani ya nchi kupitia siasa
“Sidhani kama itakuwa ni heshima mzee umeshikwa ‘Tanganyika jeki’ na mtoto mdogo, huko ni kudhalilishwa, wazee mnatakiwa kuwa washauri wa hawa vijana wanaotumia siasa vibaya na matokeo yake kuharibu amani ya nchi,”
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa