Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere, ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoani Rukwa kwa kuvuka lengo la makusanyo ya mapato kwa asilimia 120 kwa Robo ya kwanza ya Mwaka 2024/2025.
Mheshimiwa Makongoro ameyasema hayo katika Mkutano wa kwanza wa Mwaka 2024/2025 wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini uliofanyika Ukumbi wa Nazareth Mkoani Rukwa.
Katika kipindi cha Robo ya kwanza ya Mwaka wa fedha 2024/2025 Mamlaka ya Mapato Mkoa wa Rukwa imekusanya kiasi cha shilingi bilioni 12, ikilinganishwa na lengo lililowekwa la bilioni 10.
Akizungumza katika kikao hicho Mheshimiwa Makongoro amesisitiza juhudi zaidi ili kuiwezesha Serikali kufanikisha miradi mbalimbali ya kimkakati mkoani Rukwa.
Mheshimiwa Makongoro ametumia mkutano huo kuwahamasisha wafanyabiashara kuendelea kutimiza wajibu wa kulipa kodi kwa mujibu wa Sheria, ili kusaidia maendeleo ya nchi.
Kikao hicho kimehudhuriwa na mameneja wa Kanda kutoka Mikoa ya Ruvuma, Iringa, Mbeya, Songwe na Rukwa, na kimejadili mikakati ya pamoja ya kuboresha ukusanyaji wa mapato katika Kanda ya Kusini.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa