Katika kuimarisha juhudi za mapambano dhidi ya malaria nchini, Mkoa wa Rukwa unadhamiria kugawa chandarua kwa kila mwanafunzi.
Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ameyasema hayo wakati akifungua kikao cha maandalizi ya Kampeni ya Ugawaji wa vyandarua kwa wanafunzi wote Mkoani Rukwa leo Oktoba 19, 2023.
Mheshimiwa Makongoro ameeleza kuwa maambukizi ya malaria Mkoani Rukwa yamepungua kwa kiasi kikubwa kutoka asilimia 17 hadi 12% *kwa mwaka 2023* ikiwa ni matokeo ya juhudi za Serikali katika kutokomeza malaria.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa amewataka wananchi kutumia vyandarua hivyo kwa usahihi na kupiga marufuku vyandarua hivyo kutumika kwa shughuli za ufugaji, kilimo, uvuvi na matumizi yote yasiyo sahihi.
Ametaka wananchi kuendelea kuchukua hatua madhubuti za kujikinga dhidi ya malaria ikiwemo kulala ndani ya chandarua, kuharibu mazalia yote ya mbu kwa kufyeka vichaka vyote, kufukia madimbwi ya maji na kufunika vizuri vyombo vya kuhifadhia maji.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ametoa rai kwa Wakurugenzi wa Halmashauri kutenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za kuzuia malaria ikiwemo kuhakikisha vituo vyote vya afya katika Mkoa wa Rukwa vinakuwa na dawa za SP za kutosha na kuzigawa kwa kina mama wajawazito na kuwapatia vyandarua wanapofika kliniki.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa