Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere amesema kuwa anakubaliana na kauli mbiu ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi iliyotolewa katika Sikukuu ya Wafanyakazi 2024. Amesema kuwa kwa kawaida ubora wa maslahi ya watumishi unaongeza mzunguko wa fedha na kukuza uchumi wa wananchi.
Ametoa kauli hiyo leo tarehe 01 Mei 2024 alipohutubia wafanyakazi katika maadhimisho ya kimkoa ya siku ya wafanyakazi 'mei mosi' yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Laela 'A' iliyoko Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga.
Mheshimiwa Makongoro amesema kuwa Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt Samia Suluhu Hassan imekuwa ikiboresha maslahi ya watumishi kila mwaka kadri uchumi unavyoruhusu .
Amewaomba watumishi kuwa wavumilivu kuhusu suala la kikotoo kwa wastaafu kwa kuwa Serikali inatambua na kuthamini mawazo ya wadau yanayotolewa kuhusu suala hilo.
Maadhimisho ya siku ya wafanyakazi hufanyika tarehe 1 Mei, ya kila Mwaka ambapo Mwaka huu 2024 maadhimisho hayo kitaifa yamefanyika Jijini Arusha yakiwa na kauli mbiu isemayo "nyongeza ya mshahara ni msingi wa mafao bora na kinga dhidi ya hali ngumu ya maisha"
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa