Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewatoa hofu mawakala wa mbolea mkoani Rukwa kutokana na kupata changamoto ya kulipishwa kibali cha kuingiza malori katika mji w Sumbawanga huku akiwaelewesha wakulima wa mkoa huo kuwa rangi ya mbolea isiwarudishe nyuma wao kutumia mbolea bali waangalie kilichomo ndani ya mbolea hiyo.
Amesema kuwa wananchi wasiangalie rangi kwakuwa awali walizoe mbolea ya kupandia aina ya DAP ikiwa na rangi nyeusi na sasa inaletwa ya rangi nyeupe na hivyo kuwafanya wakulima hao kukosa imani na rangi hiyo na hivyo kushindwa kuitumia hali itakayopelekea kushindwa kufikia lengo la kilimo chenye tija ndani ya Mkoa.
“Kiutaalamu ile rangi siyo hoja, hoja ni kemikali ambazo zipo kwenye ile mbolea yenyewe, mbolea ambayo tunayo kwa mwaka huu ni nyeupe na wakulima wetu walizoea kuiona ikiwa katika rangi nyeusi kwahiyo wanakuwa wanasita, nitoe wito kwamba wasisite kuwa kinachojalisha ni kemikali, kemikali zipo sahihi isipokuwa rangi ambayo haina uhusiano na kemikali,” Alisisitiza
Aidha, amewaondoa hofu mawakala wa mbolea katika Mkoa wa Rukwa kwa kuwahakikishia kupewa vibali maalum na Manispaa ya Sumbawanga kwaajili ya kuingiza malori ya mbolea katika maghala yao ambayo yapo katikati ya mji wa Sumbawanga.
“Kwa vile ni hitaji kubwa la mbolea sasa hivi Wasitozwe “fee” yoyote wanapokuwa wanakwenda kupakua hii mbolea, kwasababu ukiweka vipingamizi zaidi, matokeo yake mbolea itapanda bei, ikipanda bei itamuathiri sana mkulima lakini pia na walaji, kwahiyo kwa hawa ambao yanakwenda kwenye magodown ambayo yanafahamika na yatahakikiwa yatapewa vibali vya kushusha mbolea kule kwenye magodown,” Alisema.
Mh. Wangabo ameyasema hayo baada ya kufanya ziara katika maghala 7 yanayomilikiwa na mawakala hao yaliyopo katika mkoa na kupokea malalamiko juu ya ushuru wanaotozwa shilingi 50,000/= na Manispaa ya Sumbawanga ili kuweza kupitisha malori yao katikati ya mji.
Wakati Mawakala wao wakiwasilisha changamoto na malalamiko yao mmoja wa mawakala hao Mkurugenzi wa Ikuwo General Enterprises Sadrick Malila alisema kuwa wananchi wengi wamekuwa wakidanganywa na wafanyabiashara wa mbolea ambao hununua mbolea ya kupandia DAP nyeupe na kuimwagia Kaboni na kuwa nyeusi na kuwauzia wakulima.
“Wanachokifanya wanachukua hii wanamwaga wanapuliza kaboni inakuwa nyeusi halafu wanawapiga wakulima sasa hii ni hatari sana, nimewaeleza mara nyingi kwamba tangazeni kwenye redio maana ile hata kuuza wanauza kwa kificho, kwasababu watu wanaakili ya kuwa DAP nyeusi ndio inayofanya kazi lakini sio kweli hiyo ndio chnagamoto kubwa tuliyonayo,”Alisema.
Nae Meneja wa kampuni ya ETG Hassan Habibu alisema kuwa changamoto kubwa waliyonayo ni kutozwa shilingi 50,000/= na Manispaa ya Sumbawanga hali inayorudisha nyuma nguvu za mawakala wa mbolea kuingiza mbolea kwa wingi katika mkoa wa Rukwa.
“Kumekuwa na changamoto iitwayo “off loading and loading fee” ambapo gari la uzito wa zaidi ya tani saba wanatakiwa kulipa shilingi 50.000/= hii nadhani nimeona kwenye mkoa huu, wakati wa kushusha hapa na ili iingie mjini lazima ilipe shilingi 50,000/=, kwahiyo imetuletea changamoto kubwa sana wasafirishaji kugoma kuja,” Alilalamika.
Kwa upande wake Afisa Kilimo wa Mkoa wa Rukwa Ocran Chengula alisema kuwa Mkoa umejipanga vizuri katika kuhakikisha unazalisha mazao mbalimbali zaidi ya milioni 1.7 ambapo kati ya hizo mahindi ni zaidi ya tani 700,500 na kuwa Mkoa umejipanga kuona malengo hayo yanafikiwa katika uzalisha na kuwatoa hofu wakulima juu ya upatikanaji wa pembejeo.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa