Mbio za Mwenge wa Uhuru Mwaka 2025 zimeendelea leo Septemba 30,2025 katika Wilaya ya Kalambo, mkoani Rukwa, huku miradi mbalimbali ya maendeleo ikiendelea kuzinduliwa,kukaguliwa na kuwekewa mawe ya msingi.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa Mwaka 2025, Ndg. Ismail Ali Ussi, amesema kuwa Serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha changamoto zinazowakabili wananchi katika sekta za elimu na maendeleo ya jamii zinatafutiwa ufumbuzi wa kudumu.
Akizungumza wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi katika Shule ya Sekondari Mbuluma, wilayani Kalambo, Ndg Ismail Ali Ussi amesisitiza kuwa uwekezaji katika elimu ni msingi wa maendeleo endelevu ya taifa. Amesema ujenzi wa shule hiyo ni hatua muhimu ya kuwawezesha watoto wa kike na wa kiume kupata elimu katika mazingira rafiki na salama.
Wananchi wa kijiji cha Mbuluma wameeleza kufurahishwa kwao na ujenzi wa shule hiyo, wakisema kuwa itapunguza kwa kiasi kikubwa changamoto za mimba na ndoa za utotoni. Wamesema awali wanafunzi walilazimika kutembea zaidi ya kilomita 20 kwenda shule ya kata jirani, hali iliyosababisha wengi wao kukata tamaa ya kuendelea na masomo.
Mbali na sekta ya elimu, kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge ameweka jiwe la msingi katika daraja la Mto Mao. Kabla ya kuanza kwa ujenzi wa daraja hilo hali ya maisha ya wananchi ilikuwa hatarini hasa nyakati za mvua, kutokana na kukosa miundombinu imara ya kuvukia. Wananchi wa eneo hilo wamesema kuwa kukamilika kwa daraja hilo kutapunguza ajali na vifo, na pia kufungua fursa za kibiashara kwa kurahisisha usafirishaji wa bidhaa ndani na nje ya wilaya hiyo.
Jumla ya miradi nane yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.9 imezinduliwa, kukaguliwa na kuwekewa mawe ya msingi katika Wilaya ya Kalambo kupitia Mbio za Mwenge wa Uhuru Mwaka huu. Miradi hiyo inajumuisha sekta za elimu, miundombinu na maendeleo ya jamii.
Mwenge wa Uhuru umeendelea kuwa chombo cha kuhamasisha mshikamano wa kitaifa, uzalendo na uwajibikaji, huku ukimulika kwa ukaribu utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa