Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi Mh. Kangi Lugola ameamua kutumia gereza la Mollo lililopo kata ya Mollo, Sumbawanga mjini kufanya kipindi cha “Tunatekeleza” kinachorushwa na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) kuonyesha utekelezaji wa agizo la rais Dkt. John Pombe Magufuli la kutaka magereza kuanza kujilisha.
Amesema kuwa anakwenda kwenye gereza hilo la Mollo ili kuwahabarisha watanzania yaliyofanywa na Wizara hiyo katika kipindi cha miaka mitatu ya utawala wa awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli
“Gereza la Mollo ni gereza lenye ardhi nzuri na ya kutosha, lina ekari zaidi ya 12,000 ukilinganisha na magereza mengine Tanzania, gereza la Mollo linaweza kuwa ndio kitovu cha kuanzia huu uzalishaji, kukiwa na miundombinu na vitendea kazi vya kutosha,” Mh. Lugola alisema.
Mbali na nia yake ya kufanya kipindi hicho katika gereza hilo, alitumia nafasi ya uwepo wake katika mkoa wa Rukwa Kuzungumza na kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na kugusia maeneo kadhaa ambayo alitoa tahadhari kwa kamati hiyo kuwa makini kutokana na kukuwa kwa kasi kwa Mji wa Sumbawanga na Mkoa kwa ujumla.
Miongoni mwa maeneo aliyoyagusia ni kuwasihi wananchi kuwa wepesi kushirikiana na vyombo vya usalama katika kutoa taarifa za kiuhalifu ili kuendelea kuuweka mji katika hali ya usalama na pia kuitaka Kamati ya Ulinzi na usalama kushughulikia malalamiko ya wananchi yanayotokana na kero za vyombo vya ulinzi na usalama.
“Malalmiko yafanyiwe kazi kuliko kusubiri sisi mawaziri kuja kutatua kero za maeneo haya, na maeneo ya msisitizo ni pamoja na wananchi kutobambikizwa kesi, wananchi kunyimwa dhamana ilhali wanamakosa ambayo yanadhaminika, na nimekemea mambo ya rushwa katika vyombo vya usalama na wananchi watoe taarifa za rushwa,” Alisisitiza.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa