Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Nyakia Ally Chirukile amewataka wananchi wa Wilaya ya Sumbawanga kuchangia gharama za huduma za maji ili kuifanya miradi ya maji iliyojengwa kuwa endelevu.
Mheshimiwa Nyakia amesema hayo leo Ijumaa tarehe 31 Mei, 2024 wakati akifunga Mkutano Mkuu wa Vyombo vya Watoa Huduma za Maji Ngazi ya Jamii Wilaya ya Sumbawanga kwa Mwaka 2024.
Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ametoa pongezi kwa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kwa kuvisimamia Vyombo vya Watoa Huduma za Maji na kuvipongeza vyombo hivyo kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maji.
Amesema kuwa changamoto zilizopo hazina budi kutafutiwa suluhisho la kudumu na kuomba ushirikiano kati ya viongozi wa Mkoa, Wilaya na wataalam wa maji ili kuzikabili kikamilifu.
Ametoa wito wa wadaiwa wa ankara za maji kuzilipa kwa wakati ili kuviwezesha Vyombo hivyo kujiendesha huku akitaka miradi iliyosimama kukamilishwa kwa haraka.
Awali, wajumbe wa kikao hicho waliwasilisha changamoto za uendeshaji wa miradi hiyo huku changamoto kubwa ikitajwa kuwa wananchi kushindwa kuchangia gharama za kupatiwa huduma za maji.
Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa 85% ya wakazi wa vijijini wanapata maji safi na salama ifikapo 2025
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa