Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere, amefanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo Wilayani Nkasi leo Novemba 19, 2025, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kufuatilia utekelezaji wa miradi na matumizi sahihi ya fedha za umma.
Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Makongoro amekagua maendeleo ya miradi inayotekelezwa katika sekta za afya, elimu, maji na utawala, huku akiwataka wasimamizi kuhakikisha kazi zote zinafanyika kwa viwango vinavyokubalika na kwa kuzingatia maelekezo ya Serikali. Amesisitiza kuwa nidhamu ya matumizi ya fedha, ufuatiliaji wa karibu na kasi ya utekelezaji ni msingi muhimu wa kufanikisha malengo ya Serikali.
Katika sekta ya elimu, Mkuu wa Mkoa ametembelea Shule ya Sekondari Milundikwa ambako ujenzi wa madarasa na majengo ya msingi unaendelea. Aidha, ametembelea ujenzi wa miundombinu ya kidato cha tano katika Shule ya Sekondari Chala pamoja na ujenzi wa Shule ya Amali ya Mkoa. Amesema ni muhimu kuhakikisha ubora wa kazi, upatikanaji wa vifaa kwa wakati, na kukamilika kwa miradi ndani ya muda uliopangwa ili wanafunzi wapate mazingira bora ya kujifunza.
Ametoa maagizo ya kuongeza kasi katika maeneo yote ambayo utekelezaji bado unasuasua. Akizungumza na watendaji na wananchi waliokusanyika katika maeneo mbalimbali ya ukaguzi, Mheshimiwa Makongoro amepongeza ushirikiano unaooneshwa katika kusukuma mbele miradi ya maendeleo. Amehimiza jamii kuendelea kulinda miundombinu inayojengwa na kuitumia kwa manufaa ya wote.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa amehitimisha ziara yake kwa kukagua ujenzi wa Kituo cha Afya Chala na kutembelea mradi wa maji wa Namanyere pamoja na ukarabati wa ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi. Ziara hiyo imelenga kuimarisha uwajibikaji, kuongeza ufanisi wa usimamizi wa miradi na kuhakikisha kila fedha ya Serikali inaleta matokeo chanya kwa wananchi wa Mkoa wa Rukwa.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa