Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere, amesema kuwa maandalizi ya kupokea Mwenge wa Uhuru mwaka 2025 katika Mkoa wa Rukwa yamekamilika kwa kiwango cha kuridhisha, na amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mapokezi hayo kama ishara ya mshikamano na kuunga mkono juhudi za maendeleo.
Akizungumza na vyombo vya habari leo Septemba 26, 2025 ofisini kwake, Mheshimiwa Makongoro ameeleza kuwa Mkoa wa Rukwa unatarajia kuupokea Mwenge wa Uhuru siku ya Jumapili, tarehe 28 Septemba 2025, katika Kijiji cha Kizi, Kata ya Paramawe, Tarafa ya Namanyere, Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi.
Amesema kuwa Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika Halmashauri zote nne za Mkoa wa Rukwa kuanzia tarehe 28 Septemba hadi 1 Oktoba 2025, ambapo utakimbizwa umbali wa kilomita 653.1. Katika kipindi hicho, Mwenge wa Uhuru utakagua, utaweka mawe ya msingi, na kuzindua jumla ya miradi 34 ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni 55.3.
Mheshimiwa Makongoro pia ametumia fursa hiyo kuwasihi wananchi wote waliojiandikisha na wenye sifa za kupiga kura kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa amani na utulivu. Amesisitiza kuwa kupiga kura ni haki ya kikatiba ya kila mtanzania, na ni njia halali ya kushiriki katika kuamua mustakabali wa taifa.
Aidha, ameeleza kuwa ushiriki wa wananchi katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru si tu ni ishara ya uzalendo, bali pia ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa Rukwa.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa amewahimiza viongozi wa Serikali, taasisi mbalimbali na wananchi kwa ujumla kuendelea kushirikiana katika kuhakikisha kuwa mapokezi ya Mwenge wa Uhuru 2025 yanakuwa ya mafanikio makubwa na yenye kuhamasisha mshikamano wa kitaifa.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa