Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Charles Makongoro Nyerere, ameziagiza Halmashauri zote ndani ya Mkoa kutenga maeneo maalum kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya Polisi katika kila Kata, ikiwa ni mkakati wa kuimarisha usalama wa wananchi na mali zao.
Akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa jengo la Kituo cha Polisi cha Kata ya Chala, wilayani Nkasi, uliofanyika Septemba 20, 2025, Mheshimiwa Makongoro ameeleza kuwa usalama wa wananchi ni kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Katika hotuba yake, Mheshimiwa Makongoro ametaka kila Halmashauri kuhakikisha inatenga ardhi yenye hati miliki kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya Polisi, akisisitiza kuwa maeneo hayo hayapaswi kubadilishiwa matumizi bila idhini ya Serikali.
Aidha, amewaasa wananchi wa Kata ya Chala kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuimarisha usalama, akisisitiza kuwa jeshi hilo si adui wa wananchi bali ni chombo muhimu cha ulinzi wa raia na mali zao.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Shadrack Masija, ametoa onyo kali kwa watu wote watakaojihusisha na vitendo vya hujuma dhidi ya miundombinu ya Jeshi la Polisi, akibainisha kuwa Serikali inatumia rasilimali nyingi za walipa kodi katika ujenzi na uboreshaji wa vituo hivyo.
Mradi wa ujenzi wa Kituo cha Polisi Chala umegharimu shilingi milioni 115, na unatarajiwa kutoa huduma kwa zaidi ya wananchi 68,000 wa Kata ya Chala pamoja na vijiji na maeneo jirani.
Wananchi waliohudhuria hafla hiyo wameipongeza Serikali kwa hatua hiyo, wakieleza kuwa kituo hicho kitasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza matukio ya uhalifu yaliyokuwa yakiripotiwa mara kwa mara katika maeneo ya pembezoni mwa Kata hiyo.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa