Na _Khadija Dalasia-Rukwa_
Katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya awamu ya Sita, Mkoa wa Rukwa umeshuhudia maendeleo makubwa katika Sekta ya Elimu. Kiasi cha shilingi bilioni 64.7 zimetumika kujenga na kuimarisha miundombinu ya elimu ya Msingi, Sekondari, Vyuo vya Kati na Elimu ya Juu.
Jumla ya shule mpya 36 za Msingi na Sekondari zimejengwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, Halmashauri za Wilaya za Kalambo, Nkasi, na Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga.
Mkoa wa Rukwa umepokea kiasi cha shilingi bilioni 15.3 kwa ajili ya elimu ya Msingi na shilingi bilioni 26.1 kwa ajili ya elimu ya Sekondari katika kipindi hicho. Ujenzi na maboresho ya miundombinu ya elimu kwa ujumla umepunguza changamoto ya umbali na msongamano wa wanafunzi kwa miundombinu michache iliyokuwepo. Pamoja na hayo Serikali imeboresha mazingira ya upatikanaji wa elimu.
Aidha, upanuzi wa taasisi za elimu katika ngazi zote, kama vile ujenzi wa miundombinu mipya katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya Tawi la Rukwa, ujenzi wa miundombinu mipya ya Chuo cha Ualimu Sumbawanga na ujenzi wa Chuo cha Veta Mkoani Rukwa unaendelea kuthibitisha dhamira ya Serikali ya kutanua wigo wa utoaji wa elimu kwa wananchi wake. Jumla ya shilingi bilioni 23 zimewekezwa na Serikali kwa maboresho hayo.
Matokeo ya uwekezaji mkubwa katika Sekta ya Elimu Mkoani Rukwa yameanza kuonekana. Idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa katika ngazi mbalimbali imeongezeka.
Katika kipindi cha miaka mitatu ya uwekezaji huo idadi ya wanafunzi walioandikishwa kujiunga na elimu ya msingi imeongezeka kutoka 46,526 kwa Mwaka 2021 hadi 63,666 kwa Mwaka 2024 sawa na ongezeko la asilimia 36 huku idadi ya wanafunzi waliojiunga na elimu ya Sekondari ikiongezeka kwa asilimia 9 kutoka wanafunzi 315,887 Mwaka 2021 hadi kufikia 346,787 kwa Mwaka 2024.
Ongezeko hilo ni matokeo ya mpango wa elimu bila malipo na maboresho makubwa ya miundombinu.
Kwa ujumla, Mkoa wa Rukwa umeshuhudia mabadiliko makubwa katika Sekta ya Elimu katika kipindi cha Mwaka 2021 mpaka 2024. Mabadiliko hayo yanaithibitisha nia ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuweka mazingira bora ya kujifunza na kujifunzia ili kuinua kiwango cha elimu na ujuzi kwa wananchi.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa