Mkuu wa mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo ameagiza mkuu wa shule ya sekondari Muhama Manispaa ya Sumbawanga Mkoani Rukwa kuchukuliwa hatua kwa tuhuma za kuwatoza wanafunzi michango ya Sh5,000 kama gharama ya kuwapatiwa fomu za maelezo ya kujiunga na shule hiyo.
“Hili suala la kuchangia maendeleo halikuanza jana wala juzi lakini suala hili limeporwa na viongozi wa shule, nao wanafanya kama mitaji yao, wananchi tunawaambia wachangie kwa hiyari yao lakini waelekeze kwa Mkurugenzi na sio kiongozi yeyote wa shule. Nakuagiza mkurugenzi kuchukua hatua katika hili na ninataka nipate taarifa’,” alisema.
Na kusisitiza kuwa ili kuwaepusha wazazi na michango Halmashauri hazina budi kuhakikisha kuwa zinaongeza vyanzo vya mapato ili kusaidia miradi mbalimbali ya ujenzi inayoendelea kwenye halmashauri hizo.
Mh. Wangabo ametoa agizo hilo wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara kata ya Malangali baada ya baadhi ya wananchi kufichua jambo hilo, walipopewa ruhusa ya kueleza kero zao na Mkuu huyo wa mkoa.
Mmoja wa wananchi hao, Sadock Kalinga amesema wazazi wamekuwa wakichangishwa kiasi hicho cha fedha ili wapatiwe fomu hizo.
“Tulilazimika kutoa fedha hizi na kupewa stakabadhi kwa kuwa tuliambiwa mwanachi ambaye hatotoa fedha hawezi kupewa fomu hizo na hivyo kukosa sifa ya kujiunga katika shule hii,” amesema Kalinga.
Baada ya kupokea malalamiko hayo na kuonyeshwa risiti iliyotolewa kama ushahidi, Wangabo amemhoji Mkurugenzi wa Halmashauri ya manispaa ya Sumbawanga, Hamidu Njovu kuhusu uhalali wa mchango huo ambapo naye alikana kufahamu jambo hilo.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa