Meneja wa Wakala wa barabara (TANROAD) Mkoa wa Rukwa Mhandisi Msuka Mkina ameeleza kuwa miongoni mwa changamoto zinazorudisha nyuma ujenzi na matengenezo ya bararabara za mkoani humo ni uwepo wa shughuli za kibinadamu kando ya barabara hizo.
Amesema kuwa uswagaji wa mifugo barabarani husababisha uharibifu mkubwa katika muda mfupi jambo ambalo linarudisha nyuma juhudi za serikali katika kuhakikisha inafikisha miundombinu ya barabara katika maeneo yote ya nchi.
“Upitishwaji au uswagaji wa mifugo barabarani hasa ng’ombe ni kitendo ambacho kisababisha uharibifu mkubwa katika barabara tena katika muda mfupi ni tatizo ambalo tunakabiliana nalo hivyo tunawaomba ushirikiano wa viongozi katika kutoa elimu na changanomoto nyingine ni shughuli za kibinadamu zinzzofanywa kwenye vyanzo vya mito kama vile kilimo ambapo mvua ikinyesha huleta athari kubwa,tunaomba sheria ya mazingira itiliwe mkazo” Alisema.
Ameyasema hayo katika kikao cha bodi ya barabara kilichowahusisha wabunge, wakuu wa wilaya, wenyeviti wa halmashauri, wakurugenzi wa halmashauri, kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa, wataalamu wa ofisi ya mkuu wa mkoa pamoja na mkuu wa mkoa ambaye ndiye mwenye kiti wa kikao hicho.
Katika kulithibitisha hilo makamu mwenyekiti wa kikao hicho ambae pia ni mbunge wa jimbo la Kwela, Wilaya ya Sumbawanga Mh. Ignus Malocha amesema kuwa kuna umuhimu wa kuingia mikataba na viongozi wa vijiji ama kata ili kudhibiti hali ya uzururaji wa mifugo na kuongeza kuwa sio rahisi kwa wakala wa barabara nchini (TANROAD) kusimamia maeneo hayo.
“Nilichokiona hatujaweka mkazo wa kuwabana viongozi waliopo katika maeneo hayo katika kusimamia suala hili la mifugo, jingine ni uharibifu wa mazingi ambapo kuna maeneo unaona kabisa kwamba hatujawajibika ipasavyo mfano ukitoka mtowisa kuja kijiji cha bwando eneo lote lina bonde, mwanzo kulikuwa na kalavati moja lakini kutokana na uharibifu wa mazingira sasa hivi kumekuwa na vivuko zaidi ya vinne na bado tutaendelea maana ukiangalia eneo lote limelimwa,” Alibainisha.
Meneja wa Wakala wa barabara (TANROAD) Mkoa wa Rukwa Mhandisi Msuka Mkina akitoa taarifa ya TANROAD Mkoa wa Rukwa
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kikao hicho ambae pia ni mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amezishukia halmashauri juu ya utendaji mbovu wa kudhibiti mifugo hiyo huku akiwasisitizia wakurugenzi kusimamia sheria za mifugo zilizopo kuanzia katika ngazi ya vijiji ili walipa kodi wa kitanzania waweze kufaidi matunda ya kodi zao katika ujenzi wa barabara.
“Watanzania wanalipa kodi zao, fedha ni nyingi sana, tunazipeleka kwenye miundombinu na kule ambako hakuna tunasikia hapa, kwamba jamani tunahitaji barabara Fulani TARURA barabara Fulani TANROAD lakini udhibiti wa barabara unakuwa sifuri, hiuli jambo nisingependa liendelee na iwe agenda tupate taarifa na tuambiwe namna walivyodhibiti, sio kusema tu kwamba tutafanyia kazi, tusikie wapi barabara imeharibiwa na halmashauri imedhibiti namna gani,”Alisistiza.
Katika mwaka wa fedha 2018/2019 shilingi bilioni 13.8 zimeidhinishwa kwaajili ya matengenezo ya barabara na madaraja na bilioni 2.7 kwaaajili ya miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Rukwa.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa