USTAWI WA FAMILIA UNATEGEMEA LISHE BORA- RC SENDIGA
Na. OMM Rukwa
Halmashauri za mkoa wa Rukwa zimesema zitaendelea kuhakikisha zinatenga na kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji afua za lishe ili kukabiliana na tatizo la udumavu na utapiamlo kuathiri afya ya watoto chini ya miaka mitano
Akizungumza kwa niaba ya madiwani wa mkoa wa Rukwa, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Sumbawanga Justin Malisawa alisema wakiwa wasimamizi wakuu wa halmashauri watahakikisha kila robo mwaka fedha za afua za lishe zinatengwa na kutolewa kwa jamii.
Malisawa amesema hayo leo (Oktoba 19, 2022) mjini Sumbawanga wakati wa hafla ya utiaji saini mikataba ya utekelezaji afua za lishe kati ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga na Wakuu wa Wilaya za Sumbawanga, Nkasi na Kalambo.
“Sisi madiwani tutaendelea kuhakikisha kila matumizi ya halmashauri ya miezi mitatu fedha za lishe zinatengwa na kupelekwa katika utekelezaji wa agenda za lishe .Suala la lishe endelevu litaendelea kupewa kipaumbele”alisema Malisawa.
Akifungua kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga aliwataka wakuu wa wilaya kuhakikisha mikataba waliyosaini inakwenda kutekelezwa hadi ngazi ya chini kwa watendaji kabla ya ifikapo Oktoba 25 mwaka huu.
Sendiga alibainisha kuwa mkataba huo ni maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kunakuwa na utekelezaji wa afua mbalimbali za lishe katika jamii ili kupunguza kiwango cha udumavu ambacho mkoa wa Rukwa ni asilimia 47.9.
“Maelekezo yangu kwa Wakuu wa Wilaya, mkasimamie wilaya zenu kuhakikisha fedha zilizopangwa kutekeleza afua za lishe zinatolewa kwa wakati. Aidha, taasisi zote zinazoshughulikia suala la lishe katika mkoa zijulikane ili iwe rahisi kufuatilia mipango yao utekelezaji “alisisitiza Sendiga.
Naye Mratibu wa Mradi wa Lishe Endelevu mkoa wa Rukwa Maria Machilu alisema suala la vikao vya kamati za lishe lipewe kipaumbele kwenye halmashauri ili kuwezesha jamii kushiriki kupanga mikakati ya kupunguza udumavu ikiwemo elimu ya lishe bora.
Mkoa wa Rukwa katika tathmini ya lishe iliyofanyika jijini Dodoma Septemba 30 mwaka huu ilitangazwa kushika nafasi ya kwanza kitaifa kwa utekelezaji mzuri wa afua za lishe.
Mwisho
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa