Miradi 11 yenye thamani shilingi Bilioni 56.7 imekaguliwa na Kamati ya Siasa ya Mkoa ya Chama cha Mapinduzi Wilayani Kalambo.
Kamati hiyo iliyoongozwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Rukwa Bi Silafu Jumbe Maufi imekagua ujenzi wa Miradi 02 ya Maji katika Vijiji vya Singiwe na Kalaela yenye thamani ya Shilingi Bilioni 16, Ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami barabara ya Matai - Kasesya na Matai - Kisungamile yenye thamani ya Shilingi Bilioni 37.8.
Miradi mingine ni mradi wa ujenzi wa miundombinu ya Hospitali ya Wilaya ya Kalambo ( wodi ya wazazi) yenye thamani ya shilingi milioni 250, Ujenzi wa Vituo viwili vya Afya vya Samazi na Legezamwendo vyenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.2, mradi wa ujenzi wa shule mbili mpya za Msingi za Matai na Kalepula zenye thamani ya shilingi Bilioni 1.2.
Kamati hiyo imekagua pia mradi wa ujenzi wa vyumba nane vya madarasa Shule ya Sekondari Mambwe yenye thamani ya Shilingi Milioni 160 na mradi wa skimu ya umwagiliaji wenye thamani ya shilingi milioni 202.
Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Rukwa imempongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha utekelezaji wa miradi hiyo.
Kamati ya Siasa ya Mkoa imeipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo, RUWASA, TARURA na TANROADS kwa usimamizi mzuri wa miradi.
Aidha Kamati hiyo imewataka wakandarasi kuhakikisha miradi ya maendeleo wanayoitekeleza kuikamilisha kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa ili kutimiza malengo ya Serikali kuboresha na kusogeza huduma karibu na wananchi.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa