Mwenge wa Uhuru wa Tanzania unaratajiwa kuweka mawe ya msingi, kukagua na kuzindua miradi yenye thamani ya shilingi 20,499,194,866 Mkoani Rukwa ikiwemo miradi ya maendeleo 43 na vikundi 48 katika kutekeleza malengo ya serikali ya awamu ya tano nchini.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo alipokuwa akisoma hotuba ya mapokezi ya mwenge huo wa Uhuru katika Kijiji cha Kizi, Wilayani Nkasi mpakani mwa Mkoa wa Rukwa na Katavi.
Mh. Wangabo alibainisha kuwa katika fedha hizo wananchi wamechangia shilingi 654,373,600, halmashauri zikiwa zimechangia shilingi 323,187,500, na serikali kuu nayo ikiwa imechangia 15,958,184,766 huku wadau wengine wakiwa wamechangia shilingi 3,563,499,000.
Aidha Mh. Wangabo alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Katavi kwa kumaliza kukimbiza mwenge ukiwa salama na kuwatunza wakimbiza mwenge na kuingia katika MKoa wa Rukwa wakiwa na afya nzuri na kumuhakikishia kuukimbiza mwenge huo wa uhuru kwa amani na usalama katika kipindi chote ukiwepo katika Mkoa wa Rukwa
“nikuhakikishie kuwa Wakimbiza Mwenge wote wa Kitaifa mliotukabidhi tutawalea, tutawatunza na kuwaenzi na kuhakikisha kuwa wanahitimisha Mbio za Mwenge katika Mkoa wetu kwa amani na utulivu.” Alisema.
Mwenge wa uhuru wa mawaka huu ukiwa umebeba kauli mbiu ya ‘Elimu ni ufunguo wa maisha; Wekeza sasa kwa maendeleo ya Taifa letu’ Mh. Wangabo amesema kuwa wanafunzi waliojiunga na darasa la kwanza kwa shule za msingi wamevuka maoteo ambapo wanafunzi 50,887 sawa na asilimia 106, huku wanafunzi wa shule ya awali wakifikia 39,486 ambayo ni sawa na asilimia 92 ya maoteo.
Mkoa wa rukwa ni mkoa wa sita kutembelewa na mwenge wa uhuru tangu kuwashwa kwake mkoani Geita mwanzoni mwa mwezi wa ne mwaka huu, na kutegemewa kukimbizwa kwa zaidi ya kilomita 721 katika Halmashauri nne ndani ya mkoa wa Rukwa.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa