Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amemshauri Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga kuhakikisha anakamilisha miundombinu ya barabara na mahitaji muhimu katika mradi wa upimaji viwanja katika Kijiji cha Nambogo ili kuwavutia wanunuzi na matokeo yake kupata wateja kwa haraka kuliko hali ilivyo sasa.
“Miundombinu mbalimbali mkaisogeza, huduma za maji, umeme, kunajiuza kwenyewe, hapa ni karibu na barabara na kuko bize kwenda Mbeya kuliko upande huu wa kwenda Mpanda, hakikisheni mnaweka vibanda vya biashara na kituo cha basi na mhakikishe kuwa kituo hicho kinafanya kazi basi hivi viwanja vitajiuza vyenyewe na havitatosha, hivyo cha kwanza kuhakikisha miundombinu ya msingi ipo kisha patajiuza penyewe,” Alisisitiza.
Mradi huo wenye jumla ya viwanja 2161 vilivyopimwa katika eneo la Nambogo na Katumba Azimio vimetengwa maalum kwa matumizi mbalimbali ikiwemo makazi, biashara, shule, huduma za afya, maofisi, “Shopping Mall”, vituo vya mafuta, viwanja vya michezo na maeneo ya kupumzikia. Mradi ambao tayari umeshagharimu Tsh. 1,589,692,000.
Afisa Ardhi manispaa ya Sumbawanga Thadeo maganga amesema kuwa lengo la mradi huo ni kuwa mji wa kisasa utakaokuwa na huduma mbalimbali ili kupunguza msongamano wa kufuata huduma katika eneo la kitovu cha mji kwa siku za usoni na kuonheza upatikanaji wa viwanja vilivyopimwa na kuwekewa miundombinu ya msingi na hivyo kupunguza kasi ya ujenzi holela.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbwanga amesema kuwa tayari wameshaanza kupokea maombi ya mahitaji ya viwanja hivyo na kuwataka wananchi kuendelea kujitokeza ili kuongeza kasi ya ujenzi wa nyumba kwa maeneo hayo mapya na kuweza kutanua mji huku akibainisha juhudi zinazofanyika za kuongea na benki ya NMB kwaajili ya kuwakopesha wananchi ili waweze kumudu ununuzi wa viwanja hivyo.
“hapa tunazungumzia viwanja 2161 ni mradi mkubwa ambao NMB wanaweza wakakopesha, tupo katika mijadala ya awalai ambapo tunataka “tu-twist” sheria yao “wanayo-mortgage” mpango wa ujenzi, lakini lazima uwe umeshaanza kujenga, ila si tunawaambia hawa hawajaanza lakini waone jinsi gani ambavyo wanaweza, tunawasiliana makao makuu kama wataiona hii ni fursa ya waombaji 2000 ambao tunaweza tukaingia nao mkataba mdogo na NMB ili waweze kuwakopesha wanunue wakwatwe polepole ili kuufanya huu mji uwende kwa kasi,” Alimalizia.
Jumla ya viwanja 1997 vitauzwa kwa bei elekezi ambapo kwa kila mita moja ya mraba kwa makazi pekee ni 2,700/=, makazi na biashara 3,000/=, biashara 5,000/=, huduma za jamii 3,500/=, ibada/kuabudu 3,500/=, hoteli, vituo vya mafuta na maduka ya kiuwekezaji 5,000/=.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa