Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka wananchi wananchi wa kijiji cha Kisumba, Wilayani kuhakikisha hawaitumii mizinga waliyopewa na Wakala wa huduma za Misitu (TFS) kinyume na azma ya mizinga hiyo na matokeo yake iwe chachu ya kujitengenezea mizinga mingi zaidi ili kupata asali nyingi na kuondokana na umasikini.
Aidha amewataka wanakijiji hao kuhakikisha hawazibi njia za tembo katika kuweka mizinga ya nyuki kuwazuia, kwani kwa kufanya hivyo kunaweza kusababisha madhara zaidi, na kuwatakaka kuwashirikisha wataalalmu wa wanyamapori ili kujua njia wanazopita tembo na kuziacha.
“Kelele za mivumo ya nyuki ndizo zinazowafukuza tembo na si mzinga. Mizinga tuliyowapeni na kuitundika kwenye mpaka wa Hifadhi ya msitu wa Kalambo na kijiji chenu, isitumike kama hirizi ya kutisha tembo wanaowasumbua bali mnawajibika kuhakikisha ina makundi ya nyuki mazuri na makubwa kuweza kufanikisha azma yenu.” Alisema Wangabo.
Mh. Wangabo ameyasema hayo alipokuwa akisoma hotuba kwa niaba ya mgeni rasmi Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mh. Japhet Hasunga kwenye maadhimisho ya siku ya kutundika mizinga kitaifa Iliyofanyika katika wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa tarehe 03 oktoba 2018.
Katika hotuba hiyo Mh. Wangabo alieleza fursa kadhaa zinazopatikana Katika ufugaji nyuki, zinazoweza kuifikisha nchi katika uchumi wa viwanda na hivyo kuwahimiza wananchi kuhakikisha wanazitumia fursa hizo ikiwemo kuanzisha kiwanda cha kutengeneza zana za ufugaji nyuki kama mizinga na mavazi ya kinga dhidi ya nyuki, kiwanda cha kuchakata na kufungasha na kuyaongezea thamani mazao ya nyuki kama asali, nta, gundi ya nyuki na mengineyo.
“Mojawapo ya faida nyingine za ufugaji nyuki ni kwamba hauhitaji mtaji mkubwa sana na wakati huohuo, raslimali muhimu za ufugaji nyuki tunazo tayari kama; nyuki wenyewe, mimea ya nyuki na watendaji yaani wafugaji nyuki. Kinachohitajika hapa ni elimu zaidi ya ufugaji nyuki.” Alisisitiza.
Awali akisoma taarifa kwa Mgeni rasmi Mkurugenzi msaidizi uendelezaji ufugaji nyuki Allen Kazimoto alisema kuwa Tanzania ina takriban ya hekta milioni 48.1 za misitu ambayo ingeweza kutoa tani 138,000 za asali na tani 9,200 za nta.
“Kutokana na changamoto mbalimbali ni tani 34,000 tu za asali huzalishwa kwa mwaka sawa na asilimia 26 ya uwezo wa uzalishaji na baadhi ya changamoto hizo ni usimamizi na utunzaji dhaifu wa makundi ya nyuki na teknolojia duni au isiyosahihi katika kutengeneza zana za kuhifadhia nyuki hasa mizinga,” Kazimoto alisema.
Maadhimisho hayo yenye kaulimbiu inayosema; “Tuwalinde nyuki watunufaishe katika kilimo na uhifadhi” imeonesha uhitaji mkubwa wa wataalamu wa ufugaji wa nyuki kwani waliopo katika halmashauri hawatoshelezi huku Mkoa wa Rukwa wenye hekta 147,917 za misitu na wenye uhitaji wa watalaamu wa nyuki 86, una watumishi 12 tu ambao wanategemewa katika halmashuri nne za Mkoa.
Katika maadhimisho hayo Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) waligawa mizinga ya nyuki 100 kwa vikundi vipya vitano vya waathirika wa uvamizi wa tembo katika kata ya kisumba.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa