Licha ya kuwa Mkoa wa Rukwa ni wa pili katika uzalishaji wa chakula kitaifa lakini wakulima mkoani humo wanatumia zana duni kuzalisha mazao na hivyo kuwa na kipato kisichoendana na nguvu wanazotumia kuzalisha.
Serikali ya mkoa wa Rukwa kwa kushirikia na Kampuni ya Agricom Africa Limited imeanza hamasa kwa wakulima ili waanze kutumia zana za kisasa katika kilimo kwa kuanzia wametoa mkopo wa matrekta kwa wakulima 10 ili kuwongeza uzalishaji na kuinua kipato chao.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa kampuni ya Agricom Philipo Kulaya alisema kuwa kampuni hiyo ilianza kwa kutoa mafunzo kwa wakulima waliokidhi vigezo vya kupewa mkopo huo juu ya umuhimu wa kutumia zana za kisasa na kuachana na zana za asili.
“Kupitia kampuni ya Agricom Africa Limited chini ya mwamvuli wa Serikali kwa kuwatumia maafisa ushirika, maafisa zana ambao walikuwepo kwenye hii hafla, tulichokifanya sisi ni kuwaelimisha na kuwafahamisha utofauti wa kutumia majembe ya mikono, jembe la ng’ombe na trekta” Alisema.
Aidha, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Ocran Chengula alisema kuwa matumizi ya zana za kisasa za kilimo yataongeza uchumi wa wakulima hali itakayopelekea kuongeza uchumi wa taifa na kuwa na chakula cha kutosha.
“Kwa takwimu zilizopo kutoka wizara ya kilimo mkoa wa Rukwa ni wa pili kwa uzalishaji wa chakula, upatikanaji wa matrekta haya yaliyoletwa na Agricom ni mkombozi mkubwa sana, uchumi wa mkoa wa Rukwa kwa asilimia 90 ya wananchi wanategemea kilimo, kwahiyo tunaamini kwamba hizi trekta zikienda mashambani na kuanza kulima na wakulima wakizingatia maelekezo ya maafisa ugani, tutapata mazao mengi na watu watauza na uchumi wetu utakuwa,” Alisisitiza.
Kwa upande wake Mgeni Rasmi katika hafla hiyo fupi ya makabidhiano ya matreka hayo kwa wakulima Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule aliishauri Kampuni ya Agricom Africa Limited kuweza kuwa na vipuri karibu ili wakulima watakapopatwa na shida ya uharibifu wa matrekta hayo basi iwe rahisi kutengenezwa.
“Hakikisheni kuwa aina zote za vipuri hitajika, kulingana na aina ya trekta zilizopo, vinakuwepo kwa wakati wote, vipuri vyote muhimu viwepo hapa Sumbawanga, ili hawa waliopata mkopo huu waweze kufika kwa urahisi na kuweza kupata huduma hiyo,” Alisema.
Kati ya Vyama vya wakulima 166 vilivyoomba kupatiwa mkopo katika halmashauri nne za mkoa wa Rukwa ni vyama 88 tu ndivyo vilivyopita kwenye mchujo wa kupatiwa mkopo wa trekta na hivyo ndivyo pekee vitakavypatiwa mkopo huo kwa fedha taslimu na kwa mkopo.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa