Sumbawanga.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere, ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga kwa kufanikisha ujenzi wa Shule Mpya ya Msingi Pwela kwa kutumia shilingi milioni 130 kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Shule hiyo mpya ipo katika Kitongoji cha Pwela, Kijiji cha Nambogo, Kata ya Milanzi, na inajumuisha madarasa sita, vyumba viwili vya ofisi za walimu, pamoja na matundu kumi na mbili ya vyoo.
Ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na uongozi wa shule katika kutunza miundombinu hiyo ili idumu na kuwanufaisha vizazi vijavyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga, Bi. Upendo Mangali, alisema ujenzi huo ni sehemu ya mkakati wa Halmashauri kuboresha elimu kwa kusogeza huduma karibu na wananchi, hasa wa maeneo ya pembezoni.
Wananchi wa Pwela wameeleza furaha yao, wakisema watoto wao sasa watapata elimu kwa mazingira bora na kwa umbali wa karibu.
Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Makongoro ametembelea na kukagua pia miradi mingine ikiwemo ukamilishaji wa bwalo la chakula Shule ya Sekondari Kizwite, ujenzi wa nyumba za watumishi Shule ya Sekondari Mazoezi, ukamilishaji wa jengo la wazazi Hospitali ya Isofu, ujenzi wa Kituo cha Afya Senga na ujenzi wa Uwanja wa Ndege Sumbawanga
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa