Na Khadija Dalasia, Rukwa
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere, ametoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Rukwa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika tarehe 29 Oktoba 2025.

Ametoa wito huo leo, Oktoba 27, 2025, akisisitiza umuhimu wa kudumisha amani, mshikamano na utulivu wakati wote wa mchakato wa uchaguzi ili kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa mafanikio.
Kwa mujibu wa Ibara ya 5 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2024, kila raia mwenye sifa kisheria ana haki na wajibu wa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa viongozi wa ngazi mbalimbali za uongozi.
Mheshimiwa Makongoro amesema Serikali imeweka mazingira wezeshi kuhakikisha wananchi wote wanapata fursa ya kushiriki katika uchaguzi huo kwa uhuru, usalama na amani. Aidha, amebainisha kuwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametangaza tarehe 29 Oktoba 2025 kuwa siku ya mapumziko ya kitaifa ili kutoa nafasi kwa wananchi wote kushiriki kikamilifu katika kupiga kura.
Amehimiza wananchi wa Rukwa kufika vituoni mapema siku ya uchaguzi wakiwa na vitambulisho vyao vya mpigakura, kufuata maelekezo ya maafisa wa uchaguzi na vyombo vya ulinzi na usalama, pamoja na kuepuka vitendo vyovyote vinavyoweza kuvuruga utulivu na amani katika jamii.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa ameeleza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga ipasavyo kuhakikisha uchaguzi unafanyika katika mazingira salama na ya utulivu katika maeneo yote ya Mkoa wa Rukwa.
Aidha, amekumbusha wananchi kuwa uchaguzi ni nyenzo muhimu ya maendeleo na sio chanzo cha migawanyiko, hivyo amewataka kuendelea kudumisha umoja na mshikamano baada ya uchaguzi. Ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kuutumia uchaguzi kama fursa ya kuchagua viongozi bora watakaosimamia maendeleo ya Taifa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Kwa ujumla, wito huo umetolewa ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa kampeni za uhamasishaji wa wananchi kote nchini kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa amani, umoja na uzalendo.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa