Na Khadija Dalasia - Rukwa, Agosti 2025
Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) imewakabidhi zaidi ya mizinga 200 ya kisasa ya nyuki kwa Machifu wa Mkoa wa Rukwa ikiwa sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa kuendeleza Sekta ya Ufugaji Nyuki ujulikanao kama “Achia Shoka, Kamata Mzinga”.
Akikabidhi mizinga hiyo kwa Machifu wa Wilaya ya Sumbawanga, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii anayeshughulikia Uhifadhi, Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba, alisema mpango huo unalenga kuongeza uzalishaji wa asali nchini kutoka tani 33,861 za sasa hadi tani 75,000 ifikapo Juni 2035.
“Ugawaji huu unaunga mkono juhudi za Mhifadhi namba moja nchini, Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameendelea kuwainua wananchi kiuchumi kupitia uhifadhi wa maliasili hususan misitu na nyuki,” alisema CP. Wakulyamba.
Aidha, aliwataka Machifu na wananchi kushirikiana na wataalam wa Wizara katika kujifunza mbinu za kisasa za ufugaji nyuki na kuhakikisha rasilimali hizo zinahifadhiwa kwa vizazi vijavyo. Pia aliitaka TFS kuimarisha ulinzi wa maeneo ya hifadhi na kuendeleza shughuli za utalii.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Msalika Makungu, alisema kwa sasa mkoa una jumla ya mizinga ya kisasa 5,710, mizinga ya kienyeji 2,251 na wafugaji 3,736, hivyo mizinga hiyo mipya itaongeza tija katika sekta ya ufugaji nyuki.
Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki wa Wizara hiyo, Daniel Pancras, alibainisha kuwa sekta ya ufugaji nyuki inachangia ajira takribani milioni 2 nchini kupitia uzalishaji, uchakataji na biashara ya asali pamoja na vifaa vya kufugia nyuki.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa