Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Cuthbert Sendiga amezindua mradi wa maji wenye thamani ya shilingi milioni mia tatu na ishirini na mbili katika Kijiji cha Kisa Kata ya Milepa iliyoko Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga. Mradi huo wa maji utahudumia vijiji vya Kisa na Talanda vyenye jumla ya vitongoji kumi na tisa.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mradi huo iliyofanyika leo tarehe 15 Mei 2023 Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita kwa kutoa fedha nyingi katika sekta ya maji na kuwatua ndoo kichwani akina mama wa Mkoa wa Rukwa.
Amewataka wananchi wa Kijiji cha Kisa na Talanda kuhakikisha wanalinda miundombinu ya maji, wanatunza vyanzo vya maji, wanaacha kulima kandokando ya mito na kutokata miti hovyo ili miradi ya maji iwe endelevu na yenye tija kwa jamii.
Ameielekeza Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kusimamia miradi ya maji kwa karibu zaidi ili ikamilike kwa wakati ili malengo ya Serikali ya kuwahudumia wananchi yafikiwe kwa ufanisi wa juu zaidi. Amesema Rukwa bila miradi viporo inawezekana.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa