MWENGE WA UHURU 2025 WAPOKELEWA MANISPAA YA SUMBAWANGA, MIRADI YA BILIONI 30.3
Mwenge wa Uhuru umeingia katika siku ya pili ya mbio zake mkoani Rukwa ambapo leo Septemba 29, 2025 umepokelewa Manispaa ya Sumbawanga.
Ukiwa Manispaa ya Sumbawanga Mwenge wa Uhuru umeweka mawe ya msingi na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 30.3
Miongoni mwa miradi iliyozinduliwa ni pamoja na ujenzi wa Soko la Mazao Kanondo, ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kupitia mradi wa TACTICS, uzinduzi wa huduma za afya katika Hospitali ya Manispaa ya Sumbawanga, ujenzi wa shule mpya ya Msingi Pwela kwa kutumia mapato ya ndani na ujenzi wa Ofisi ya Wilaya ya Wakala wa Misitu Tanzania (TFS)
Pamoja na miradi hiyo Mwenge wa Uhuru umetoa hamasa kwa wananchi juu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kitaifa za kulinda mazingira na kuboresha afya za watumiaji.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa miradi hiyo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Bw. Ismail Ali Ussi, ameipongeza Manispaa ya Sumbawanga kwa utekelezaji wa miradi hiyo kwa ubora wa hali ya juu unaoendana na thamani ya fedha na mahitaji ya wananchi. Ameeleza kuwa miradi hiyo ni kielelezo cha namna serikali inavyotekeleza dhamira ya kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.
Kaulimbiu ya Mwenge wa Uhuru kwa Mwaka 2025 ni "Jitokeze kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa Amani na Utulivu."
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa