Mwenge wa Uhuru Mwaka 2025 umepokelewa rasmi mkoani Rukwa, leo Septemba 28, 2025 katika Kijiji cha Kizi, Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi.
Mwenge wa Uhuru utakimbizwa ndani ya Mkoa wa Rukwa kwa siku nne, ambapo unatarajiwa kukimbizwa katika Wilaya tatu za Nkasi, Kalambo na Sumbawanga zenye jumla ya Halmashauri nne.
Ukiwa mkoani Rukwa Mwenge wa Uhuru unatarajia kuzindua, kuweka mawe ya msingi na kufungua jumla ya miradi 34 katika sekta za maji, elimu, afya, barabara, maendeleo ya jamii pamoja na vilabu 8 vya ulinzi wa mazingira pamoja na mapambano dhidi ya rushwa, dawa za kulevya na malaria, huku thamani ya jumla ya miradi hiyo ikiwa shilingi bilioni 55.3.
Akizungumza wakati wa sherehe za kuupokea Mwenge wa Uhuru kutoka Mkoa wa Katavi, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere amesema kuwa katika kutekeleza miradi itakayokaguliwa na Mwenge wa Uhuru mkoani Rukwa 2025, Serikali Kuu imechangia asilimia 98.58 ya fedha zote, sawa na shilingi 54,592,082,337.74. Halmashauri za Mkoa wa Rukwa zimechangia asilimia 1.12, sawa na shilingi 619,074,000.33, huku wananchi wakichangia asilimia 0.27, sawa na shilingi 150,546,500.00. Ameeleza kuwa mchango wa wahisani na wadau mbalimbali wa maendeleo ni asilimia 0.03, sawa na shilingi 14,417,000.00.
Mheshimiwa Makongoro amewashukuru wananchi na wadau wa maendeleo kwa mshikamano. Amewataka kushiriki kikamilifu katika kuchagua viongozi katika Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 29, 2025
Naye Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ndg. Ismail Ali Ussi, ameeleza kuwa mbio za Mwenge wa Uhuru Mwaka 2025 zinalenga kuhamasisha uwajibikaji wa viongozi na wananchi, kukuza mshikamano wa kitaifa na kupambana na vitendo vya rushwa, sambamba na kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
Mwenge wa Uhuru 2025, unatarajiwa kuanza mbio zake Wilaya ya Nkasi kabla ya kuendelea na mbio zake katika Halmashauri nyingine za Mkoa wa Rukwa.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa