Mwenge wa Uhuru 2025 ukiwa katika siku yake ya kwanza mkoani Rukwa, umeweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Amali wilayani Nkasi, hatua inayolenga kuimarisha upatikanaji wa elimu ya ufundi kwa vijana.
Akizungumza katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi leo Septemba 28, 2025, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ndg. Ismail Ali Ussi, amewataka wazazi na walezi kuwahamasisha watoto wao kusoma katika shule za amali ili kupata ujuzi wa vitendo utakaowawezesha kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
Kiongozi huyo ametumia fursa hiyo kumpongeza Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Mheshimiwa Peter Ambrose Lijualikali, pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, Bw. Afraha Nassoro Hassan, kwa kusimamia vyema utekelezaji wa mradi huo muhimu kwa maendeleo ya wananchi.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kukamilisha ujenzi wa shule hiyo kwa wakati ili ianze kutoa huduma kwa vijana waliokusudiwa ili kuleta mageuzi katika sekta ya elimu ya ufundi mkoani Rukwa.
Katika hatua nyingine, Kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa, Ndg. Ismail Alli Ussi amewapongeza wananchi wa Nkasi kwa ushiriki wao wa moja kwa moja katika shughuli za maendeleo, akieleza kuwa mshikamano huo unaonyesha dhamira ya kweli ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli.
Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kuendelea na mbio zake kesho tarehe 29 Septemba 2025, kwa kukabidhiwa rasmi kwa Manispaa ya Sumbawanga, ambapo utaendelea kukagua, kuzindua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi ya maendeleo kabla ya kuelekea Halmashauri za Wilaya za Kalambo na Sumbawanga.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa