Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi amelitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuhakikisha inakamilisha mradi wake wa ujenzi wa nyumba za Makazi za Jangwani katika Manispaa ya Sumbawanga mkoa wa Rukwa katika kipindi cha mwaka huu wa fedha 2019/2020.
Akizungumza wakati akikagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa nyumba hizo za makazi wenye jumla ya nyumba ishirini za ghorofa moja jana katika Manispaa ya Sumbawanga mkoa wa Rukwa Naibu Waziri Mabula alisema mradi huo lazima ukamilishwe mapema kwa kuwa fedha iliyotumika ni nyingi.
Kauli hiyo ya Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi inafuatia kuelezwa na Mkuu wa mkoa wa Rukwa Joachim Wangabo kuwa mradi huo umekuwa ukimsumbua kutokana na kuchukua muda mrefu bila kukamilika na hivyo kuufanya mkoa kutojua hatma yake wakati uhitaji wa nyumba za kupanga katika manispaa ya Sumbawanga ni mkubwa.
‘’ Naungana na RC kuwa mradi huu umechukua muda mrefu hivyo ni lazima uishe katika mwaka huu wa fedha wa kiserikali na April mwaka huu 2020 narudi hapa Sumbawanga’’ alisema Dkt Mabula.
Kwa mujibu wa Meneja Mawasiliano wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Muungano Saguya, mradi huo wa ujenzi wa nyumba za Makazi Jangwani katika Manispaa ya Sumbawanga ulianza mwezi Juni 2014 na ulisimama kupisha uchunguzi baada ya kuwepo tuhuma za ubadhilifu kwenye mradi huo.
Hata hivyo, Saguya alisema kiasi cha shilingi milioni 366.2 kinahitahika kumalizia mradi huo na tayari Shirika lake limejipanga na maandalizi kwa ajili ya ukamilishaji mradi yamekamilika na muda wowote umaliziaji nyumba hizo utaanza.
Mradi huo wa Nyumba za Makazi Jangwani katika Manispaa ya Sumbawanga mkoa wa Rukwa ambao nyumba moja ilishanunuliwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHF) zikikikamilika zitapangishwa na zitaweza kuliingizia Shirika la Nyumba la Taifa kiasi cha shilingi 5,400,000 kila mwezi.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa