Nyumba zaidi ya 135 katika vijiji vya Kinambo, Maenje, Milepa, Sakalilo na Talanda vilivyopo kata ya Milepa na Ilemba, katika bonde la Ziwa Rukwa Wilayani Sumbawanga, Mkoani Rukwa zimeathiriwa vibaya na mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali na kuziacha kaya zaidi ya 72 zikiwa hazina mahala pa kuishi hali ilimpelekea Mkuu wa Mkoa huo Mh.Joachim Wangabo kufika katika maeneo hayo kuwafariji na kutoa mkono wa pole kwa waathiriwa wa janga hilo.
Katika Salamu zake za pole kwa waathiriwa hao Mh. Wangabo alisema kuwa janga hilo hakuna aliyelitegemea na kulifananisha tukio hilo na ajali ambayo haina king ana ndio sababu iliyopelekea kufika hapo kutoa pole kutokana na janga hilo na kuwapongeza wale waliowahifadhi ndugu na jamaa ambao wamekosa mahala pa kuishi kutokana na nyumba zao kuangushwa na mvua hiyo.
“Ninajua hapa kuna familia ambayo haina mahali pa kuishi lakini pia kuna watu ambao wamekwisha hama makazi yao, wamefadhiliwa na ndugu jamaa na marafiki, mimi nimependa sana hii kwamba janga limetokea watu wa kwanza kuwasaidia waliopata hayo maafa ama majanga ni ninyi wenyewe ndani ya vijiji, huo ndio utu na uzalendo tunaoutaka, tusaidiane tuwe na moyo wa kusaidiana, leo limemkuta mwenzako kesho litakukuta wewe, usipomsaidia huyu na wewe hutosaidiwa,” Alisema.
Aidha, katika ziara yake yake hiyo alitoa kilo 500 za unga wa sembe pamoja na kilo 200 za maharage kwa kamati ya maafa ya wilaya ili waweze kugawa kwa waathiriwa wa mvua hiyo katika vijiji hivyo vya bonde la Ziwa Rukwa na kuwataka wadau mbalimbali kuweza kujitokeza kusaidia waathiriwa hao ili waweze kurudi katika maisha yao ya kawaida.
Miongoni mwa wananchi walioathirwa na mvua hizo waliweza kutoa sababu za mvua hizo kuharibu majengo yao huku wakiisisitiza serikali kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi juu ya namna ya kujenga nyumba bora na imara zitakazoweza kuhimili upepo mkali ikiwemo kuweka Linta kwenye nyumba zao pamoja na kufunga makoa yanayoweza kushikilia bati zisiachane na kuta za nyumba zao, Deus Kibona wa Kijiji cha kinambo alisema.
“Tunajenga nyumba ilimradi tu na wengine hawazimalizi, nyumba ikishajengwa yaani mtu kusema afunge makoa, hafungi anaacha kwahiyo ndio kinachangia, ingekuwa angalau tunakumbuka hata kuweka linta lakini hata linta hatukumbuki kupiga linta, mtu akishapiga bati anaona tayari ameshajenga nyumba mambo mengine anajisahau ndio maana maafa yanaendelea kutokea, kwahiyo naiomba serikali ingetoa maagizo kwa wale wanaojenga nyumba kutoa tahadhari ya kufunga makoa yaani hata wakaguzi wangekuwa wanapita ingekuwa angalau”.
Aidha lisema kuwa mbali na mvua hiyo kuharibu nyumba pia zimeharibu mshamba ya wakulima wengi wa vijiji hivyo baada ya mafuriko na upepo mkali kulaza mahindi yaliyokuwa yanaelekea kukomaa kwaajili ya kuvuna.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa