Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI, Wizara ya Maendeleo ya Jamii na Taasisi ya WAJIBU imeanza mafunzo maalum kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii na Maafisa Ununuzi ili kuwawezesha kuibua na kusajili Makundi Maalum kwenye mfumo wa ununuzi wa umma (NeST).
Mafunzo hayo yameshirikisha Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa wa Rukwa, wawezeshaji kutoka PPRA na TAasisi husika, Maafisa Ununuzi wa Halmashauri, Maafisa wa Wilaya na Kata pamoja na waandishi wa habari.
Akifungua mafunzo, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Ndg. Marwa Wankyo, amesema Serikali inalenga kuhakikisha wafanyabiashara wadogo na wajasiriamali wananufaika na fursa za Sheria Mpya ya Ununuzi wa Umma ya 2023, inayozitaka Taasisi nunuzi kutenga asilimia 30 ya mpango wa ununuzi kwa Makundi Maalum. Amesisitiza watendaji kutumia mafunzo hayo kuwafikia walengwa, kuwaelimisha juu ya uundaji na usajili wa makundi kupitia mfumo wa PPRA, na kuongeza idadi ya makundi yatakayoshiriki kwenye zabuni za Serikali.
Mafunzo haya yameelezwa kuwa muhimu katika kuongeza uwezo wa Makundi Maalum kushindana na kupata tenda, hivyo kuinua kipato na kukuza uchumi wa wananchi. Baadhi ya Maafisa Maendeleo ya Jamii wameishukuru Serikali na PPRA wakisema mafunzo yamewaongezea uelewa na kuwasaidia kutatua changamoto walizokuwa wakikumbana nazo. Wamewahimiza wanawake, vijana, watu wenye ulemavu na wajasiriamali wadogo kujitokeza kusajili makundi yao na kunufaika na fursa za zabuni za Serikali
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa