Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Benard Makali amewasisitiza wanakamati ya elimu na maendeleo ya ushirika ya mkoa kuhakikisha kuwa wanatekeleza majukumu yao ya kufikisha elimu ya ushirika kwa wananchi ili iwanufaishe katika maisha yao ya kila siku.
Ameyasema hayo alipokuwa akiziindua kamati hiyo yenye wajumbe 10 kutoka katika halmashauri za Mkoa na sekta binafsi ili kuimarisha utendaji kazi na kuhakikisha kuwa leimu hiyo inasambazwa katika ngazi zote.
“Hii ndiyo kamati ambayo itafufua ushirika, watu wakishaelewa maana ya ushirika watajiunga kuanzia maofisini hadi mitaani kuna watu ambao wngependa kujiunga lakini hawana elimu ya kustosha juu ya dhana ya ushirika,” Makali alisema.
Amewataka kuwa makini na vyama vinavyomea na hatimae kuwa na idadi kubwa bila ya kufanya kazi, hali inayoonyesha mpaka sasa mkoa una idadi ya vyama 166 na vinavyofanya kazi ni vichache na kuongeza kuwa vyama vinavyoendeshwa kwa ufanisi ndio vinavyohitajika na sio wingi wake.
Awali alipokuwa akisoma risala kwa mgeni rasmi, afisa wa ushirika wa Mkoa, Wallace Kiama alitaja baadhi changamoto zinazowakabili ikiwamo vitendea kazi pamoja na upungufu wa watumishi hasa katika ngazi ya halashauri jambo ambalo linawafanya kushindwa kufanya kazi zao kwa ufanisi.
Katika kulijibu hilo katibu tawala wa Mkoa amesema kuwa anazitambua changamoto hizo na kuahidi kuzishughulikia kwani baadhi ya changamoto hizo zipo ndani ya uwezo wake na kuwataka ili elimu hiyo iwafikie wananchi kwa haraka waandae mada hiyo ambayo atawahitaji kuiwasilisha katika vikao vya maendeleo vya mkoa.
Zaidi ya hayo aliitaka kamati hiyo kuhakikisha kuwa vyama vyote vinaendeshwa kwa kufuata sheria na kanuni za vyama vya Ushirika kwa ajili ya ufanisi.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa