Katibu tawala wa Mkoa wa Rukwa Bernard Makali amewatawaka wakuu wa idara za ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kuongeza kasi katika utendaji wao wa kazi za kila siku ili kukamilisha kazi wanazoagizwa kwa wakati na kuziwasilisha taarifa kwa wakati.
Aliyasema hayo alipokuwa akifungua kikao cha mafunzo ya kiongozi cha utaratibu wa mafunzo elekezi ya awali kwa watumishi wapya wa Sekretarieti za mikoa na mamalaka za serikali za mitaa yanayoendeshwa kwa ushirikiano wa Ofisi ya Rais – Tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) na mradi wa Uimarishaji Mifumo ya Sekta za Umma (PS3)
“Wakuu wa Idara wanatakiwa wawe makini katika semina hii ya siku moja, wazingatie haya wanayofundishwa ili wawe msaada kwa watumishi wapya serikalini lakini pia watumishi waliopo kwenye idara zenu, hiki mnachokipata hapa kiwe na faida kwa wote kisibaki kwenye makabrasha yenu tu,”Alisema.
Mafunzo hayo ambayo yanajumuisha wakuu wa idara ni maalum kwaajili ya kuwaongezea uelewa wakuu hao ili kuimarisha utendaji kazi wao pamoja na watu wanaowaongoza kwenye idara zao ili kuwa na utendaji mzuri unaozingatia maadili katika kazi.
Lakini pia alipongeza mradi wa Uimarishaji Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) kwa kutoa mafunzo hayo hasa kwa wakati huu ambapo serikali inaendelea kuajiri na kupata watumishi wapya ambao watafaidika na uelewa wa wakuu hao wa idara na kuwafundisha watumishi hao.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa