SENDIGA: ‘NI AIBU RUKWA KUENDEKEZA IMANI ZA KISHIRIKINA’
Na. OMM Rukwa
Mkuu wa Mkoa Queen Sendiga akemea kikundi cha matapeli kilichoibuka mkoani humo maarufu kama rambaramba ambao wanasababisha taharuki kwenye jamii wakisaka washirikina.
Ametoa onyo hilo leo (Alhamisi, Novemba 03,2022) wakati wa mkutano wa hadhara na wananchi wa kijiji cha King’ombe kata ya Kala wilaya ya Nkasi ambapo kwa siku za hivi karibuni matapeli hao wamekuwa wakichangisha fedha ili waondoshe ushirikina.
Sendiga ametoa agizo hilo kufuatia hivi karibuni kutokea kikundi cha watu wanaofanya utapeli kwa kupita kwenye makazi ya watu na kusaka wachawi hatua inayopelekea taharuki kwenye wilaya za Nkasi, Kalambo na Sumbawanga.
“Mnaharibu sifa nzuri ya mkoa wetu, watu wanakimbia nyumba zao kwa kuogopa rambaramba kufika kusaka wachawi. Kata hii inaongoza kwa kufanya vikao vya kusaka wachawi. ” alisema Sendiga.
Katika mkutano huo, Sendiga ametoa agizo kwa Jeshi la Polisi kuendesha msako na kuchukua hatua za kuwafikisha mahakamani watu wanaoendeleza vitendo vya kusaka wachawi kwenye makazi ya watu.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Peter Lijualikali amemhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa ataongoza kampeni maalum ya kuwasaka watu wanaofanya utapeli kwa kigezo cha kusaka wachawi kwenye makazi ya watu na kukusanya fedha kwa watu.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amefanya ukaguzi wa vituo vya afya Kate na Kala ambavyo vimepokea kila kimoja shilingi Milioni Mia Tano (500,000,000) zilizotokana na tozo ambapo ameagiza Halmashauri kuhakikisha vituo hivyo vinakamilika kabla ya mwaka 2022 kuisha.
Mwisho.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa