Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen amewashauri waandishi wa habari Mkoani Rukwa kuandika habari ambazo zitasaidia kuutangaza Mkoa kwa manufaa ya nchi na wananchi hasa katika sekta za uwekezaji.
Ameyasema hayo alipokutana na waandishi hao leo (tarehe 3/4/2017) ili kuona namna ambayo wanaweza kuutangaza Mkoa na kuweza kukaribisha uwekezaji katika Mkoa wa Rukwa.
“Jambo hili la Kuutangaza Mkoa ni la kwetu sote, na hamuutangazi Mkoa kwa manufaa ya Mkuu wa Mkoa au Katibu Tawala wa Mkoa bali ni kwa manufaa yetu sote, hivyo nawaomba mtakayoyafanya na kuyaandika yawasaidie wananchi wa Rukwa” Mkuu wa Mkoa alishauri.
Mkuu wa Mkoa aliongeza kuwa ipo haja ya kuutangaza Mkoa wa Rukwa kwakuwa watu hufikiri Mkoa huu upo pembezoni mwa nchi na ni kwa ushirikiano na waandishi pekee ndio unaweza kuuweka Mkoa katika nafasi nzuri katika mioyo ya watu.
“Wawekezaji wengi ninaokutana nao hawaifahamu sana Rukwa, na mara nyingi hutembea na ramani kama njia mojawapo ya kuwaonesha Rukwa ilipo na mambo mazuri yanayopatikana katika Mkoa wetu, ila naendelea kusema kuwa ushirikiano wenu ni muhimu sana,” Mh. Zelote alisisitiza.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa