Sumbawanga, Rukwa
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere, ameipongeza Benki ya Biashara Tanzania (TCB) kwa kuendelea kuimarisha huduma za kifedha nchini, wakati wa uzinduzi wa jengo jipya la benki hiyo Sumbawanga.
Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa Jengo hilo iliyofanyika leo Julai 10, 2025, RC Makongoro amesema kuwa uzinduzi wa jengo hilo ni ushahidi wa dhamira ya benki hiyo katika kusaidia maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi, hasa wajasiriamali wadogo, wa kati na wakubwa, wanawake na vijana hususan waishio vijijini.
"Tukio hili la kihistoria linaashiria mafanikio makubwa ya benki hii, na hatua muhimu kuelekea ujumuishi wa huduma za kifedha, ukuaji wa uchumi, na maendeleo ya Taifa," alisema RC Makongoro.
RC Makongoro ameishukuru TCB kwa kuguswa na changamoto za kijamii mkoani Rukwa kwa kusaidia sekta za elimu na afya, akisisitiza kuwa huo ni mfano wa taasisi inayowekeza katika ustawi wa jamii.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa TCB, Bw. Adam Mihayo, amewahakikishia wananchi kuwa benki hiyo itaendelea kutoa huduma bora na bunifu ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya kiuchumi na teknolojia nchini. Ameleza kuwa Benki imetenga kiasi cha shilingi bilioni 20 kwa ajili ya kuwakopesha wajasiriamali.
Uzinduzi huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, wafanyakazi wa TCB na wananchi wa Sumbawanga waliokuwa na hamasa kubwa kushuhudia tukio hilo la kihistoria.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa