Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere Mkuu wa Mkoa wa Rukwa amefungua Semina ya Uwekezaji leo Agosti 20, 2024.
Semina hiyo imefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kuhudhuriwa na wawakilishi wa taasisi za fedha, wadau mbalimbali wa sekta ya biashara, na wawekezaji wa ndani Mkoani Rukwa.
Semina hiyo inayoendeshwa na maafisa kutoka Kituo cha Uwekezaji cha Taifa (TIC) ina lengo la kuhamasisha uwekezaji wa ndani ikiwa ni kampeni ya kitaifa iliyozinduliwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa kwa lengo la kuwahamasiha wananchi kufanya uwekezaji wa ndani na kuondoa dhana ya kwamba uwekezaji ni kuhusu wageni pekee.
Mheshimiwa Makongoro ameitumia fursa hiyo kuwahamasisha washiriki kuchangamkia fursa ya kujisajili katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ili kupata manufaa ya mifumo ya kikodi na kupongeza jitihada zinazoendelea za kuhamasisha Watanzania kushiriki katika uwekezaji wa ndani.
Sambamba na semina hiyo maafisa wa Kituo cha Uwekezaji wametembelea miradi ya wawekezaji wa ndani ya kiwanda cha vinywaji baridi cha Dew Drop Drinks Company Limited na kiwanda cha kuchakata mazo ya samaki cha Alfa Tanganyika Flavour Limited vyote vya Sumbawanga ikiwa ni sehemu ya hamasa kwa wawekezaji wa ndani.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa