Na Khadija Dalasia
Rukwa. 5 Mei, 2025
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere ameanza ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo Mkoani hapa.
Katika siku yake ya kwanza Manispaa ya Sumbawanga leo Mei 5, 2025, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa ameshuhudia mafundi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wakiwasha umeme katika Kijiji cha Isesa kilichoko Manispaa ya Sumbawanga baada ya kukamilisha ujenzi wa njia ya usambazaji wa umeme katika Kijiji hicho.
Akizungumza na wananchi katika Kijiji hicho Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa ameeleza kufurahishwa kwake na namna miradi ya umeme inavyotekelezwa Mkoani hapa huku akieleza kuwa zaidi ya asilimia 68 ya vijiji 1816 Mkoani hapa vimekwishaunganishwa na nishati ya umeme inayosambazwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
Mheshimiwa Makongoro amekagua pia mradi wa ujenzi wa kituo cha kupoozea umeme katika mradi wa kuunganisha umeme wa Tanzania na Zambia (TAZA) na mradi wa kuunganisha umeme katika mradi wa ujenzi wa Soko la Mazao la kimataifa la Sumbawanga na kuitaja kama mifano ya miradi inayotekelezwa kwa kasi nzuri na kwa ubora na Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO)
Ongezeko la watumiaji wa umeme katika vijiji vya Mkoa wa Rukwa linatajwa kuwa miongoni mwa mafanikio yanayochochea kuongezeka kwa biashara zinazohitaji nishati ya umeme na hivyo kuchangia moja kwa moja katika ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Rukwa.
Pamoja na miradi hiyo ya umeme, ziara ya Mkuu wa Mkoa imeangazia pia mradi ya ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Sumbawanga.
Ziara ya Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa inatarajia kuendelea tena kesho Mei 6, 2025 katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa