Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere amefanya ziara ya ukaguzi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga leo Januari 29, 2026.

Ziara hiyo ni sehemu ya ziara zake za ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali katika sekta mbalimbali mkoani Rukwa.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mheshimiwa Makongoro amesisitiza umuhimu wa taasisi za umma kuwa na hati miliki za maeneo yanakotekelezwa miradi ya maendeleo.
Amebainisha kuwa umiliki wa ardhi ni msingi wa kulinda rasilimali za umma na kuwezesha upanuzi wa huduma kulingana na mahitaji ya sasa na ya baadaye.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Makongoro ameelekeza taasisi hizo kuongeza ukubwa wa maeneo yao pale inapohitajika ili kuepuka changamoto za uhaba wa ardhi katika siku zijazo.

Vilevile, Mheshimiwa Makongoro amewaagiza viongozi wa shule na vituo vya kutolea huduma za afya kupanda miti ya matunda katika maeneo yao.
Amesema hatua hiyo itachangia uhifadhi wa mazingira pamoja na kuboresha lishe kwa wanafunzi, wagonjwa na jamii inayozunguka taasisi hizo.
Aidha, Mkuu wa Mkoa amesisitiza kuwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo uzingatie viwango vya ubora, thamani ya fedha na ukamilishaji kwa wakati.

Amesema lengo ni kuhakikisha wananchi wananufaika na huduma zinazotolewa na Serikali kwa ufanisi na kwa wakati stahiki.
Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Makongoro ametembelea na kukagua ujenzi wa madarasa katika Shule ya Sekondari Ikozi.
Pia ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Shule ya Msingi Mzindakaya na Zahanati ya Mshani.

Kadhalika, amekagua miundombinu ya nyumba za walimu katika Shule ya Wasichana Rukwa na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Zahanati ya Kavifuti.
Miradi hiyo inalenga kuboresha utoaji wa huduma za elimu na afya kwa wananchi wa Wilaya ya Sumbawanga.

Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa