Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere, amekutana na Kamati ya Amani ya Mkoa leo Novemba 20, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa (RDC) kwa lengo la kujadili namna ya kuimarisha mshikamano na kudumisha utulivu katika jamii mkoani Rukwa.
Katika hotuba yake, Mheshimiwa Makongoro amesisitiza umuhimu wa kuendeleza misingi ya umoja bila kutenganishwa na tofauti za kiimani. Ameeleza kuwa imani za dini zilizopo zinapaswa kuwa nguzo ya kuiunganisha jamii kama walivyofundisha waasisi wa taifa la Tanzania.
Aidha, Mheshimiwa Makongoro amekumbusha kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo. Ametoa wito kwa wananchi kuilinda na kuithamini amani kwa vitendo. Vilevile, ametoa wito kwa viongozi wa jamii kuendelea kuimarisha maadili, uvumilivu na upendo. Amesema kuwa tunu hizo zimeiwezesha Rukwa kubaki miongoni mwa mikoa yenye utulivu nchini.
Kikao hicho kimehitimishwa kwa makubaliano ya kuendeleza ushirikiano kati ya viongozi wa kijamii na taasisi mbalimbali ili kulinda na kukuza amani kwa manufaa ya wananchi wote wa Mkoa wa Rukwa.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa