Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa amewataka Wakandarasi wote wanaotekeleza miradi ndani ya Mkoa wa Rukwa kuikamilisha kwa ubora na kwa wakati.
Mheshimiwa Makongoro ametoa maelekezo hayo leo Mei 21, 2024 alipofanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya ujenzi katika Wilaya za Sumbawanga na Kalambo.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa amekagua miradi ya ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Sumbawanga na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kupitia mradi wa TACTICS miradi inayotekelezwa katika Wilaya ya Sumbawanga.
Miradi mingine iliyokaguliwa ni mradi wa ujenzi wa bweni la wanafunzi wenye mahitaji maalum katika Shule ya Msingi Matai 'A', ujenzi wa daraja la Mto Kalambo na ujenzi wa barabara ya Matai- Misungamile Wilayani Kalambo.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa amesema kuwa lengo la Serikali ni kuboresha huduma kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuufungua Mkoa wa Rukwa kiuchumi kwa kuiimarisha sekta ya usafiri na usafirishaji.
Mheshimiwa Makongoro amewataka wakandarasi wote kuiunga mkono Serikali kwa kufanya kazi usiku na mchana ili kuzikamilisha kwa wakati.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa