Na Khadija Dalasia.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere, ametoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi Mkoani Rukwa kuanzia Julai 2023 hadi Juni 2024.
Akizungumza katika kikao cha Kamati ya Siasa ya Mkoa, Mheshimiwa Makongoro ameeleza kuwa Mkoa umevuka lengo la ukusanyaji wa mapato kwa shilingi bilioni 17.8.
Mheshimiwa Makongoro amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa maendeleo makubwa ya Mkoa wa Rukwa huku akiwapongeza wananchi na viongozi wa Chama cha Mapinduzi na Serikali kwa ushirikiano walioutoa wakati wa ziara ya Mheshimiwa Rais Mkoani hapa Julai 2024.
Akizungumzia hali ya usalama wa Mkoa, Mheshimiwa Makongoro ameeleza kuwa hali ya usalama imeimarika na kuongeza kuwa ulinzi katika maeneo yote umeimarishwa akigusia hali ya Ziwa Tanganyika, ambako ulinzi umeimarishwa kudhibiti utekaji wavuvi.
Aidha Mheshimiwa Makongoro amezungumzia mafanikio ya sekta ya elimu yanayotokana na uwekezaji wa zaidi ya shilingi bilioni 8.2 katika ujenzi na umaliziaji wa miundombinu ya shule na ujenzi wa majengo ya Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya, Kampasi ya Rukwa.
Kuhusu Sekta ya Afya Mheshimiwa Makongoro ameeleza kuwa uwekezaji wa kiasi cha shilingi Bilioni 2.3 umefanyika katika ujenzi wa miundombinu Mkoani hapa.
Maeneo mengine yaliyoguswa katika taarifa hiyo ya Mheshimiwa Makongoro ni pamoja na Sekta ya Miundombinu ambayo imepokea Shilingi Bilioni 60 kwa ajili ya kiwanja cha Ndege, Bilioni 82.2 kwa ajili ya barabara za TANROADS, na Bilioni 8.5 za barabara za TARURA , Bilioni 20.3 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu kupitia miradi ya TACTICS na Bilioni 16.6 kwa Sekta ya maji.
Akipokea Taarifa hiyo Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Rukwa Hajjat Silafu Jumbe Maufi ametoa pongezi kwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa na wataalamu wote kwa namna wanavyoshirikiana katika utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2020-2025 na kusisitiza Halmashauri zote ziweke mipango inayoendana na mahitaji ya wananchi na kutatua changamoto zao ili kukamilisha utekelezaji wa Ilani ifikapo 2025.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa