MKUU wa Mkoa wa Rukwa, Kamishna Mstaafu Zelote Stephen amemuagiza Kaimu Mganga Mkuu wa mkoa huo, Dk Emmanuel Mtika, ahakikishe mtoto Peter Kazumba (13) anayesumbuliwa na ugonjwa sugu wa ngozi, anapelekwa haraka katika Hospitali ya Mkoa wa Rukwa iliyopo Sumbawanga mjini kwa matibabu.
Mtoto Peter ambaye hasomi anaishi na wazazi wake katika kitongoji cha Nkata kilichopo katika Kata ya Kate wilayani Nkasi, anasumbuliwa na ugonjwa sugu wa ngozi kwa zaidi ya miaka mitano bila kupona.
Aidha, Mh.Zelote aliwataka wakazi wa kitongoji hicho, kuacha kumnyanyapaa mtoto huyo pamoja na familia yake ya watu wote wanane, akiwemo baba na mama mzazi na watoto wengine watano akiwemo mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja wameambukizwa ugonjwa huo. Mh.Zelote alitoa maagizo hayo baada ya kufika katika kitongoji hicho na kujionea mwenyewe jinsi mtoto huyo anavyoteseka kwa kuugua ugonjwa huo, ambao madaktari wanadai hauambukizi.
Mkuu wa Mkoa alilazimika kufunga safari hadi katika kitongoji cha Nkata, ikiwa ni siku moja baada ya vyombo vya habari kuripoti habari ya mtoto huyo na familia yake, ambayo imetengwa na wakazi wa kijiji hicho kwa hofu ya kuambukizwa. Katika Msafara huo aliongozana na Kaimu Mganga Mkuu wa mkoa wa Rukwa, Mtika na Mratibu wa Ukoma na Kifua Kikuu mkoa wa Rukwa, Dk Dismas Buhiri.
“Acheni kuinyanyapaa familia hii wala nisisikie wanaenda kutibiwa kwa mganga wa kienyeji, hivyo namuagiza Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa (Dk Mtika) aagize gari la wagonjwa lije kumchukua mtoto huyu haraka iwezekanavyo na kumpeleka kwa matibabu ya uhakika na uangalizi na uchunguzi wa kitabibu katika Hospitali ya Rukwa ya mkoa wa Rukwa iliyopo mjini Sumbawanga,” Mkuu wa Mkoa alisema.
Pia alimtaka Dk Mtika kuhakikisha anamtuma mtaalamu wa magonjwa ya ngozi kufika katika familia hiyo na kuwafanyia uchunguzi wa kitabibu, kubaini wanafamilia wengine wapatao saba kama wanaweza kutibiwa wakiwa nyumbani kwao; au kama watalazimika nao kutibiwa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa. “Nataka maagizo yangu yatekelezwe haraka iwezekanavyo bila kuchelewa,“ alisema.
Aliwataka wakazi wa mkoa wa Rukwa, kuachana na tabia ya kuwaficha wagonjwa nyumbani kutokana na imani za kishirikina, bali wawahishe katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa matibabu. “Nawahimiza wakazi wa Kata ya Kate wajiunge na Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii (CHF) ili wasishindwe kutibiwa kwa kukosa fedha za matibabu, na nataka wakifika hospitali watibiwe haraka iwezekanavyo,“ alisisitiza.
Baba wa mtoto huyo, aitwae Martin Kazumba alimweleza Mh. Zelote kuwa yeye ndiye alikuwa wa kwanza katika familia hiyo kuugua ugonjwa huo miaka saba iliyopita, kisha mke na watoto wote sita, walifuata kwa kuambukizwa ugonjwa huo.
Kwa upande wake, Dk Mtika alieleza kuwa baada ya kumwona mtoto Peter, upo uwezekano mkubwa kwamba ugonjwa alionao ni wa ngozi au upo uwezekano kuwa familia hiyo imekula chakula, ambacho kimewasababishia mzio (allergy) na siyo ugonjwa ambao unaweza kuambukiza. Akifafanua, alieleza kuwa huo sio ugonjwa wa kuambukiza kwa sababu hakuna watu wanaoishi karibu na familia hiyo walioambukizwa.
“Mtoto Peter hatembei vizuri, anatembea kwa kuchechemea, jambo ambalo sio zuri, wataalamu wa ngozi wapo, vifaa na dawa vipo, tutampeleka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wetu ambapo atakuwa chini ya uangalizi wa wataalamu hao isitoshe atafanyiwa uchunguzi wa kitabibu,“ alisisitiza.
Mratibu wa Ukoma na Kifua Kikuu wa Mkoa wa Rukwa, Dk Buhili aliwatoa hofu wakazi wa kitongoji hicho kuwa ugonjwa ulioikumba familia hiyo, sio ugonjwa wa ukoma. Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nkata, Wilbroad Feruzi alisema anawashukuru viongozi wa mkoa huo kwa kufika katika eneo hilo na kushuhudia wenyewe jinsi mtoto Peter anavyoishi na kutoa msaada wa kumsafirisha hadi mjini Sumbawanga kwa matibabu na uchunguzi wa kitabibu.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa