Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga kuhakikisha wafanyabiashara hawafungui biashara zao bila ya kufanya usafi katika maeneo wanayofanyia biashara.
Agizo hilo lilitolewa baada ya Mkh. Zelote kufika katika soko kuu la mji wa Sumbawanga na kutokuta hata mfanyabiashara mmoja wa soko hilo akifanya usafi na huku uchafu katika eneo hilo ukiwa umekithiri katika siku hiyo ya usafi wa jumamosi ya mwisho wa mwezi maarufu kama Magufuli day.
Aidha Mh. Zelote alikuta askari wa usalama wa raia wakiendelea na usafi wa soko hilo na maeneo yanayozunguka soko hilo na kutokuwa na hata afisa mtendaji wa mtaa aliyekuwa akisimamia ama kuhamasisha usafi katika maeneo hayo hali iliyomfanya kuagiza waitwe uongozi wa mtaa na Mkurugenzi ili kuwaonya.
“Siku hii imetungiwa sharia kabisa ili watanzania wote washiriki kwenye usafi, badala yake mnalala mnategemea jeshi ndio linawafanyie kazi, kwani jeshi wameajiriwa kwasababu hiyo, wanakazi nyingi za kufanya, kama Mkurugenzi wa Manispaa ni jukumu lako kuhakikisha Manispaa inakuwa safi, kwani imekuwa nafasi ya 17 si kwasababu ya msukumo tunaoufanya bila ya hivyo ingekuwaje,” Alisema.
Amesisitiza kuwa usafi ni kila siku na jumamosi ya mwisho wa mwezi imewekwa kama ukumbusho wa kuendelea na usafi Katika maeneo yote yam ji, majumbani na kwenye maeneo ya biashara.
Katika zoezi hilo Mh. Zelote alishiriki kufanya usafi na kukagua Soko kuu la Manispaa lililopo kata ya Mazwi pamoja na Soko la Sabasaba linalomilikiwa na Chama tawala cha CCM pamoja na kusikiliza kero kadhaa za wafanyabiashara wadogo wadogo wa soko la Sabasaba.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa