Mkuu wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen ameitaka mikoa yenye upungufu wa chakula nchini kuorodhesha mahitaji yao kupitia ngazi zilizopo ili wanunue bidhaa hiyo ili kuondokana na hofu ya upungufu wa chakula nchini.
Pia aliwaomba wakuu wa mikoa kuwahamasisha wafanyabiashara wao wafike Mkoani kwake kununua bidhaa hiyo badala ya wakulima kuanza kukimbiza chakula hicho nje ya nchi, ambapo kwa msimu wa mwaka wa mavuno 2016/2017 Mkoa umevuna tani Milioni 1.1 za chakula huku zao la mahindi peke yake likiwa ni tani 710,652.
“Nichukue nafasi hii kuthubutu kuiambia mikoa mingine ambayo haijapata bahati ya kuvuna kama kama tulivyovuna sisi watumie fursa hii watuambie kupitia ngazi zilizopo kwamba wanahitaji nini, hili ni kwa Tanzania bara na visiwani, tunawakaribisha kufanya biashara na sisi,” Alisema.
Ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya kilimo cha kisasa yaliyoshirikisha uongozi wa Mkoa, Wilaya na Halmashauri zake katika shamba la Msipazi lenye ukubwa wa ekari 4,420 lililopo katika Kijiji cha China, Kata ya Kate,Wilayani Nkasi mali ya Salum Summry.
Mh. Zelote ameonya kuwa hakuna mwananchi atakayepewa chakula cha msaada kutoka serikalini kutokana na njaa, hivyo aliwaonya wanannchi wa mkoa huo kuachana na tabia ya kuuza chakula na badala yake waache akiba katika nyumba zao.
“Sisi siyo wachoyo, uchoyo wetu ni kuhakikisha wananchi wetu wanakuwa na akiba ndani ya nyumba zao, na wale wanaouza mazao wahakikishe wanatenga fedha zinazotokana na mauzo hayo kwaajili ya kununua pembejeo za msimu wa kilimo unaofuata,” Amesema.
Katika kuhakikisha wakulima wanaondokana na adha ya mbegu feki na ubabaishwaji wa bei za pembejeo Mh. Zelote amewaagiza wauzaji wa pembejeo hizo kuweka mabango ya bei nje ya maduka yao na kuwaagiza wakuu wa wilaya kuwachukulia hatua wale wote watakaogundulika kuuza mbegu feki.
Mbali na hayo Mh. Zelote amesema kuwa anataka kusikia mkoa wa Rukwa unakuwa wa kwanza nchini kwa uzalishaji wa chakula baada ya kuwa wa tatu ukitanguliwa na Ruvuma na Mbeya, hivyo aliwataka wale ambao hawalimi kuonja utamu wa kilimo kwa kulima japo ekari moja.
“Naambia Mkoa wa Mbeya umekuwa wa Kwanza, tujiulize wametuzidi nini, mkoa wa Ruvuma umekuwa wa Pili, wametuzidi nini, sasa mwaka huu nataka kusikia mkoa wa Rukwa umekuwa wa kwanza ama wote watatu tushike namba moja,” alimalizia.
Awali alipokuwa akisoma taarifa ya shammba hilo, Mkurugenzi wa Shamba la Msipazi Salum Summry amesema kuwa miongoni mwa changamoto zinazorudisha nyuma juhudi za wakulima katika Mkoa wa Rukwa ni uwepo wa mbegu zisizo na ubora “Fake” pamoja na wadudu waharibifu wa mazao.
“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa suala la mbegu feki limekuwa likirudisha nyuma juhudi zetu kama wakulima ambao tunaanza kuchipukia, na pia msimu huu tulishambuliwa na wadudu jamii ya viwavi jeshi lakini nichukue nafasi hii kukushukuru wewe binafsi, Mkuu wa Wilaya ya Nkasi pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri kwa mlivyotusaidia kukabiliana na wadudu hao kwa kuwezesha kupata ndege ya kunyunyizia madawa n ahata mafuta ya ndege kwaajili ya kazi hiyo,” Salum Summry alisema.
Naye Mstahiki Meya wa manispaa ya Sumbawanga Mh. Justin Malisawa alimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuwahamasisha wananchi wa Rukwa kulima na kuongeza thamani katika mazao yao.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa