Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen ameilipia huduma ya Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii (CHF) familia ya watu 8 ya Mtoto Peter Kazumba aliyekuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa ngozi ili familia hiyo isishindwe kupata matibabu baada ya kuruhusiwa hospitali hapo.
Mkuu wa Mkoa alitoa fedha hizo na kumkabidhi Mganga Mkuu wa Wilaya Dk. Mathias Abuya baada ya kuwatembelea watoto wawili wa familia hiyo wanaoendelea kupata matibabu katika Hospitali teule ya Wilaya ya Nkasi (DDH) na kuona ahueni kubwa aliyoipata mtoto huyo baada ya kupita siku sita tangu atoe agizo la kufanyiwa matibabu.
“Duh, sikumfahamu kabisa yaani kwakweli siwezi kuamini, mimi nilidhani ningeagiza apelekwe Muhimbili, sasa mimi nawalipia hii huduma ya CHF ili muendelee kupata huduma mtakapoendelea kuwepo hapa na baada ya kutoka hapa na pia mkawe mabalozi mkirudi huko kijijini kuwahamasisha wananchi wengine kujiunga na huduma hii,” Mkuu wa Mkoa alielezea.
Pamoja na kukabidhi fedha za CHF pia aliwaachia fedha taslim tsh. 20,000 kwaajili ya kununua chakula kwa siku hiyo na kuahidi kuwanunulia nguo watoto hao ili kuachana na nguo ambazo walikuwa wakizivaa wakati walipokuwa wanasumbuliwa na ugonjwa huo.
Mkuu wa Mkoa hakuacha kusisitiza utendaji kazi wa Serikali katika kuhakikisha wananchi wa Tanzania wanapata huduma bila ya kubaguliwa na kwa uhakika na kusisitiza kuwa wananchi wasiache kuiamini serikali na sekta ya afya na matokeo yake kuelekea kwenye mambo ya kishirikina.
“Mnaona sasa serikali inavyofanya kazi, kama isingekuwa serikali huyu mtoto asingefikia hapa, baada tu ya kupata taarifa kupitia vyombo vya habari na kuona tatizo hili, serikali imeingilia kati na matokeo yake ndio haya, bila hivyo mngeendelea kufikiria mambo mengine ambayo yapo kinyum na taratibu,” Mh. Zelote alisisitiza.
Pia alimshauri baba wa familia hiyo kuwaanzisha watoto shule baada tu ya kupona ili watoto hao waweze kujua kusoma na kuandika na kuongeza kuwa shule itawaongezea elimu ya usafi ili waendelee kujitunza.
Katika kuhakikisha familia hiyo inajikwamua katika umaskini, Mkuu wa Mkoa alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi Julius Kaondo ampeleke afisa Ugani wa kata ya Kate kwa familia ya Martin kazumba ili kumsaidia kuzalisha mazao mengi zaidi katika msimu ujao wa kilimo baada ya msimu huu kutokuwa mzuri kwa familia hiyo inayomiliki eka 7 za ardhi katika kitongoji cha Nkata.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa