Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen amekabidhi jumla ya mifuko 20 ya simenti katika shule ya sekondari Nkasi pamoja na kukabidhi mifuko 70 na mabati 100 katika Shule ya Msingi Miombo zote zilizopo katika Wilaya ya Nkasi na kufanya idadi ya mifuko 90 ambayo 40 kati ya hiyo ilitolewa na Mbunge wa Nkasi kaskazini Mh. Ali Kessy ambapo Mkuu wa Mkoa aliikabidhi kwa niaba yake.
Pamoja na kukabidhi vifaa hivyo pia Mh. Zelote aliweka jiwe la msingi katika ujenzi wa madarasa matatu ya shule ya msingi Miombo katika maadhimisho miaka 53 ya siku ya muungano ambayo kimkoa ilifanyika katika Wilaya ya Nkasi, na kitaifa kufanyika kwa mara ya kwanza katika makao makuu ya nchi, Mkoani Dodoma.
Alikabidhi vifaa hivyo ikiwa ni kuunga mkono juhudi za wananchi wa Wilaya hiyo katika kupunguza ukosefu wa madarasa unaoukabili wilaya pamoja na kuendelea kutekeleza sera ya elimu bila ya malipo iliyoanza kwa kumaliza upungufu wa madawati na sasa kuelekea katika ujenzi wa madarasa.
Akizungumza wakati kukabidhi vifaa hivyo katika shule ya Msingi Miombo Wilayani humo Mkuu wa Mkoa alisema “Wanakijiji wa Miombo ni wachapakazi wazuri na wanamuitikio katika kuchangia maendeleo kwasababu hiyo nami nawaunga mkono kwa kuongezea mifuko 50 ili nikabidhi mifuko 70 na mabati 100.”
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa