Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen amekutana na wathibiti ubora wa shule wa halmashauri nne za Mkoa wa Rukwa kujua changamoto wanazokumbana nazo na mambo yanayopelekea kushuka kwa elimu katika Mkoa.
Mh.Zelote alifikia uamuzi wa kuwaita wathibiti hao baada ya Mkoa wa Rukwa kushuka kielimu kutoka nafasi ya 6 mwaka 2015 hadi nafasi ya 12 kati ya Mikoa 31 kwa mwaka 2016 kwa mitihani ya kidato cha 4, na pia kuteremka katika mitihani ya kidato cha pili kutoka nafasi ya 20 kwa mwaka 2015 hadi nafasi ya 21 kwa mwaka 2016.
Wathibiti hao walielezea sababu kede kede zilizopelekea kushuka kwa kiwango cha elimu katika Mkoa wa Rukwa na kusema kuwa miongoni mwa sababu hizo ni kutopewa mrejesho wa taarifa za kila wiki wanazoziandika na kukabidhi kwa wakurugenzi wa halmashauri na wakuu wa wilaya.
“Toka Mwezi July mwaka jana tumeshaandika ripoti nyingi tu zinazoelezea mapungufu kama vile, upungufu wa waalimu kwa baadhi ya masomo, matundu cha vyoo, vitabu vya kusomea, nakadhalika lakini hakuna hata mrejesho tunaoupata kutoka kwa Mkurugenzi,” Goreth Ntulo alieleza.
Kwa upande mwingine sababu zinazokwamisha ufanisi wa kazi za wathibiti hao wanadai kutopewa motisha na mwajiri wao na kuwasababisha kuishi katika maisha magumu.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa